Lyon macho yote kwa Niyonzima, Msuva

Muktasari:

Ubora wa wachezaji hao kwenye mechi ya leo ambayo Yanga inahitaji kuibuka na ushindi ili irudi kileleni mwa msimamo wa ligi, ndiyo unaoweza kuibeba au kuiangusha timu hiyo leo dhidi ya Lyon.

Dar es Salaam. Haruna Niyonzima na Simon Msuva ndio wachezaji walioshikilia pointi tatu muhimu za Yanga dhidi ya African Lyon leo zitakapokutana jijini leo kwenye Uwanja wa Uhuru.

Ubora wa wachezaji hao kwenye mechi ya leo ambayo Yanga inahitaji kuibuka na ushindi ili irudi kileleni mwa msimamo wa ligi, ndiyo unaoweza kuibeba au kuiangusha timu hiyo leo dhidi ya Lyon.

Wachezaji hao wawili pekee wamehusika katika mabao tisa kati ya 10 ambayo Yanga imeyafunga katika mechi zake tano za mwisho kwenye ligi hiyo.

Wakati Msuva akifunga mabao manne na kutoa pasi mbili za mabao, Niyonzima amefunga bao moja na kutoa pasi tano za mabao katika magoli hayo tisa ambayo wawili hao wamehusika nayo.

Ni wazi kuwa Lyon inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi, inapaswa kuwachunga zaidi nyota hao wawili ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali katika siku za hivi karibuni.

Huenda Yanga leo ikamtumia kiungo wake Justin Zulu ambaye hakucheza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu kutokana na kutokuwa na kibali cha kufanya kazi nchini.

Kikwazo kwa Msuva na Niyonzima kinaweza kuwa ni kipa wa Lyon, Rostand Youthe ambaye amekuwa kigingi kwa washambuliaji wa timu pinzani pindi wanapokutana naye.

Rostand katika mechi tano za mwisho, ameruhusu mabao mawili tu kwenye mechi dhidi ya Prisons na Ruvu Shooting na amecheza mechi tatu dhidi ya Simba, Azam na Mbeya City bila nyavu zake kutikiswa.

Kipa huyo aliyeumia bega kwenye mchezo dhidi ya Azam mwishoni mwa wiki iliyopita, amepoza presha kwenye kikosi cha Lyon baada ya kuanza mazoezi mepesi juzi na bila shaka atakuwamo kwenye kikosi kitakachocheza dhidi ya Yanga leo.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi aliliambia gazeti hili kuwa kikosi cha timu yake kipo kamili kwa ajili ya kusaka pointi tatu muhimu kwenye mchezo wa leo dhidi ya Lyon.

“Tunapomaliza mchezo mmoja akili yetu tunaielekeza kwenye mchezo mwingine. Tumefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya kuikabili Lyon. Tunategemea mechi itakuwa ngumu lakini malengo yetu ni kupata ushindi,” alisema Mwambusi.

Beki wa Lyon, Hassan Isihaka alisema timu yake itahakikisha haitengenezi mianya ambayo inaweza kuwapa nafasi Yanga kuwatibulia.

“Niyonzima na Msuva ni wachezaji wa kawaida tu kama ilivyo kwa wengine. Utofauti ni kuwa wako kwenye fomu ya juu kwa sasa,” alisema Isihaka.