MO aeleza ukweli mchungu kwa Simba


Muktasari:

Dewji aliyasema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akielezea sababu iliyomfanya atangaze nia ya kutaka kuwekeza asilimia  51 ya hisa kwenye klabu hiyo kwa Sh20 bilioni.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mwanachama wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ amesema timu hiyo inatakiwa kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ili ishindane na Yanga na Azam.

Alisema kwa sasa Azam na Yanga zina nguvu kubwa ya kiuchumi na kifedha zinazowezesha timu hizo kufanya vizuri tofauti na Simba ambayo imekuwa haifanyi vyema kwa misimu minne mfululizo ya Ligi Kuu Bara.

Dewji aliyasema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akielezea sababu iliyomfanya atangaze nia ya kutaka kuwekeza asilimia  51 ya hisa kwenye klabu hiyo kwa Sh20 bilioni.

“Yanga na Azam wanatumia bajeti inayokadiriwa kuwa Sh. 2.5 bilioni kwa mwaka kila moja, wakati bajeti ya Simba ni Sh1.5 bilioni kwa mwaka ambayo ni nusu ya bajeti zao.

“Hii inasababisha Simba ishindwe kusajili wachezaji na makocha wazuri, kulipa mishahara mizuri na kutoa huduma nzuri kwa klabu kama zinavyofanya Yanga na Azam.

Alisema kwa kuwa Yanga na Azam wao bajeti yao ni kubwa, Sh2.2 bilioni, iwapo mfumo ukibadilika na watu kuanza kuwekeza, kwa mwaka tutakuwa na bajeti ya Sh5.5 bilioni zitakazo tumika katika sehemu mbili.

“Sh4 bilioni zitatumika kuendeshea timu kwa kufanya usajili, kulipa mishahara na huduma nyingine wakati kiasi cha Sh 1.5 bilioni kitatumika kutengeneza na kusimamia miundombinu kama vile uwanja wa mazoezi, kituo cha tiba, hosteli, sehemu ya mapumziko na kituo cha mikutano ya waandishi wa habari,” alisema Dewji.