Manara agoma kufungiwa

Muktasari:

Akizungumza jana muda mfupi baada ya hukumu hiyo, Manara alisema haitambui na ataendelea na shughuli zake za soka kama kawaida.

Dar es Salaam. Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara kujihusisha na shughuli za soka kwa mwaka mmoja kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu.

Akizungumza jana muda mfupi baada ya hukumu hiyo, Manara alisema haitambui na ataendelea na shughuli zake za soka kama kawaida.

Katika majibu yake, Manara alisema: “Naitumikia Simba na barua waliyotuma TFF ni kupitia anwani ya timu, kwa hiyo sikuona ajabu viongozi kujibu kwani kweli nilikuwa na dharula, sasa cha kujiuliza waliogopa nini kunisubiri hadi Jumanne na hukumu wametoa jana (Jumapili)?” Alihoji.

“Bado nitaendelea kutumikia Simba na sitasita kufanya hilo, Malinzi (Rais wa TFF) na watu wake wanafanya haya kwa faida yao na sipo tayari kuona naonewa katika hili.”

Akisoma hukumu hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Joseph Msemo alisema Manara alipatikana na makosa matatu tofauti. Kosa la kwanza ni kukashifu, kutuhumu na kuidhalilisha TFF, la pili kueneza chuki za ukabila na la tatu ni kuingilia utendaji wa TFF.

Kutokana na kupatikana na hatia, kamati hiyo imemwamuru Manara asijihusishe na shughuli za soka kwa miezi 12 na kulipa faini ya Sh9 milioni.

“Kosa la kwanza ameamuliwa kulipa kiasi cha Sh1 milioni, kosa la pili atalipa kiasi cha Sh3 milioni na la la tatu Sh5 milioni, hivyo kufanya jumla kuwa Sh9 milioni,” alisema Msemo.

“Na kama Manara ataendelea kupuza hukumu hiyo, tutafuata hukumu B ya sheria namba tatu, ambayo atafungiwa kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi kwa muda wa miaka saba,” aliongeza.

Licha ya hukumu hiyo, Msemo alisema endapo Manara ataona hajaridhika na uamuzi wa kamati yao, mlango wa kukata rufaa upo wazi.

“Akiona hajatendewa haki basi akate rufaa na kwenye kikao hakuepo angali anajua alitakiwa afike, kamati imeona kuwa hakuheshimu wito,” alisema kiongozi huyo.

Manara aliingia matatizoni katika kikao chake na waandishi wa habari akitumia muda mwingingi kuonyesha hasira yake kwa madai ya shirikisho hilo kuinyima haki Simba katika matukio mengi.

Kubwa ambalo Manara alishawishika kukutana na waandishi wa habari lilionekana pia kuchangiwa na utata wa pointi tatu za mezani ambazo Simba ilipewa licha ya kufungwa na Kagera Sugar mkoani Kagera.

Kamati ya Saa 72 ya TFF iliipa Simba pointi tatu kutokana na kubaini kuwa beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi alicheza mchezo wao dhidi ya Simba akiwa na kadi tatu za njano.

Baada ya hukumu hiyo ya kuipa Simba pointi tatu, Kagera Sugar ilipeleka malalamiko yake TFF na Kamati ya Katibam Sheria na Hadhi za Wachezaji ilikutana tena na kuhoji baadhi ya mashahidi kujiridhisha juu ya uamuzi wa awali.

Kamati iliyomfungia Manara inaongozwa na Kitwana Manara, ingawa hakuwepo jana wakati wa huku, akisaidiwa na Msemo, wakati wajumbe wengine ni Nassor Duduma na Kassim Dau.

Waliofungiwa utawala wa Malinzi ni Damas Ndumbaro (mwanasheria)- miaka saba, Jerry Muro (Ofisa Habari wa Yanga- mwaka, na Brown Ernest (Katibu Lyon)

Walifungiwa kwa kupanga matokeo

Choke Abeid (Maisha), Kipa wa Geita, Mohammed Mohammed (miaka 10), Yusuf Kitumbo na Fateh Remtula ( Maisha) na waamuzi Masoud Mkelemi, Fedian Machunde (miaka 10).