Manara aitupia vijembe Yanga

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara

Muktasari:

  • Mchezo wa Simba na Yanga ulichezeshwa na Mathew Akrama wa Mwanza na wasaidizi wake walikuwa Mohammed Mkono wa Tanga na Hassan Zani wa Arusha.

Dar es Salaam. Uongozi wa klabu ya Simba umewapongeza waamuzi waliochezesha mchezo wake dhidi ya Yanga kwamba walichezesha vizuri mchezo huo walioshinda mabao 2-1.
Mchezo wa Simba na Yanga ulichezeshwa na Mathew Akrama wa Mwanza na wasaidizi wake walikuwa Mohammed Mkono wa Tanga na Hassan Zani wa Arusha.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema klabu imeridhishwa na kiwango cha waamuzi, sisi hatutaki kubebwa tunataka mpira uchezeshwe kwa haki, lakini zaidi tumewafunga mdomo hasa huyo Mkemi (Salum).
“Kabla ya mchezo huo Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mkemi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema Yanga ni timu kimataifa na haina nafasi ya kujibishana na Simba kuhusu ligi ya ndani na alitamba kuwa wachezaji wa Yanga  wanajua umuhimu wa kuifunga Simba ili kulinda hadhi yao.
Manara alisema kelele za viongozi wa Yanga zimewatokeana puani na kuwataka kutotafuta mchawi baada ya kufungwa  na kuiacha Simba ikitulia kileleni ikiwa na pointi 54, tano zaidi ya Yanga yenye pointi 49.
Alisema, “Nawaomba kabisa wasimlaumu Lwandamina kwa kipigo hiki, waangalie hata umri wa wachezaji wao walinganishe na wa Simba.”