Mapro washindwa kuthibitisha ubora

Muktasari:

Takwimu za usajili zilizojumuishwa kutoka klabu mbalimbali nchini zinaonyesha kuwa msimu huu klabu za Ligi Kuu zimesajili wachezaji 36 wa kigeni na 26 kati yao sawa na asilimia 72, nchi zao zimefuzu kucheza fainali.

Dar es Salaam. Licha ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu kupokea wachezaji wengi wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali Afrika, wameshindwa kuthibitisha ubora wao baada sehemu kubwa kutoswa na vikosi vyao vya Taifa vilivyofuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2017).

Takwimu za usajili zilizojumuishwa kutoka klabu mbalimbali nchini zinaonyesha kuwa msimu huu klabu za Ligi Kuu zimesajili wachezaji 36 wa kigeni na 26 kati yao sawa na asilimia 72, nchi zao zimefuzu kucheza fainali.

Kati ya wachezaji hao 26, wachezaji watatu tu sawa na asilimia 11 wamepenya na kuitwa katika timu zao za Taifa zinazojiandaa na mashindano ya Afcon yanayoanza wiki moja ijayo.

Licha ya Azam FC kutia fora kuwa na nyota 12 wa kigeni, Bruce Kangwa ni mmoja wa wachezaji, ambaye anaweza kuitwa mchezaji wa kimataifa iwapo kitatumika kigezo cha kuitwa kwenye kikosi cha Taifa.

Nyota wa kigeni waliokuwa katika kikosi cha Azam FC msimu huu ni Stephane Kingue, Enock Atta Agyei, Pascal Wawa, Daniel Amoah, Samuel Afful, Yakubu Mohammed, Yahya Mohammed, Michael Balou, Ya Thomas Gonabo, Fransisco Zekumbawira, Jean Mugiraneza na Kangwa.

Simba msimu huu ilisajili nyota tisa wa kigeni, ambao ni Jean Bokungu, Method Mwanjali, Mousa Ndusha, Frederick Blagnon, Laudit Mavugo, Daniel Agyei, Vincent Angban, James Kotei, lakini ni mchezaji mmoja, Juuko Murshid aliyefaulu vigezo vya kuitwa mchezaji wa kimataifa.

Yanga msimu huu ina nyota wanane wa kigeni, Haruna Niyonzima, Amiss Tambwe, Mbuyu Twitte, Justine Zullu, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Bossuo. Lakini ni raia huyo wa Togo, Bossuo pekee aliyeitwa katika kikosi hicho cha Afrika Magharibi.

Stand United ina wachezaji wawili wa kigeni, Mnigeria Abasilim Chidiebele na Mganda Frank Muwonge, lakini hakuna hata mmoja aliyewahi kufikiriwa kuitwa hata katika kikosi cha akiba cha nchi yake.

Mbeya City ina nyota wanne kutoka nje, Tito Okello na Hood Mayanja kutoka Uganda, Sankhan Mkandawire na Owen Chaima kutoka Malawi. Chaima aliwahi kuidakia timu ya taifa ya Malawi ‘The Flames’.

African Lyon ina mchezaji mmoja wa kigeni, ambaye ni Youthe Rostand, huku Mbao FC nayo ikiwa na Alex Iwoomba, lakini wote hawana nafasi hata kwenye vikosi vya akiba vya nchi zao.

Niyonzima, Tambwe na Mavugo wangeweza kuwemo katika vikosi endapo nchi zao zingefuzu kucheza fainali hizo.

Kwa takwimu za msimu huu ni dhahiri kuwa kuna changamoto katika kupata wachezaji wa kimataifa, ambao wanaweza kutoa changamoto kwa wachezaji wazawa.

Ivory Coast imefuzu kucheza fainali hizo, lakini wachezaji wanne wanaocheza msimu Frederick Blagnon, Ya Thomas Gonabo, Vicent Angban na Michael Balou walishindwa kupenya kwenye kikosi.

Zimbabwe licha ya kuwa na wachezaji watano wanaocheza nchini msimu huu, Fransisco Zekumbawira, Method Mwanjali, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko na Gervas Kangwa. Kangwa pekee amepenya kwenye kikosi kitakachocheza fainali za mwaka huu.

Ghana, licha ya kuwa na wachezaji wanane, Daniel Amoah, Yahya Mohamed, Yakubu Mohammed, Samuel Afful, James Kotei, Daniel Agyei, Enock Atta Agyei, Alex Iwoombi na Samuel Afful, hakuna hata mmoja aliyepenya kwenye kikosi cha Black Stars.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) msimu huu imekuwa na wachezaji wawili, Mussa Ndousha na Jean Bokungu, lakini hawajaitwa kwenye kikosi cha kocha Frolent Ibenge. Cameroon ina wachezaji wawili nchini, Stephane Kingue na Youthe Rostand. Mshambuliaji wa zamani wa Simba na timu ya Taifa (Taifa Stars), Emanuel Gabriel alisema klabu kukosa sera za usajili wa wachezaji wa kigeni ndiko kumeigeuza Ligi Kuu kuwa kichaka cha wageni aliodai wengi uwezo wao hautofautiani na wachezaji wazawa.

“Viongozi wote wa klabu siyo Simba wala Yanga hawana maskauti wa wachezaji. Ifike hatua mchezaji kutoka nje awe na kitu cha ziada kuliko mchezaji wa ndani vinginevyo soka letu halitafika popote,” alisema Gabriel.

Mchambuzi wa soka na mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay alisema kukiuka maazimio ndiko kumesababisha kufika tulipo.

“Tuna azimio la Bagamoyo ambalo liliweka ‘standards’ (viwango) vinavyotakiwa kwa mchezaji wa kigeni kucheza nchini, lazima awe amecheza timu yake ya taifa na atoke katika klabu ya Ligi Kuu.

“Hizo timu zina mifumo mibovu ya usajili. Kuna mchezaji alisajiliwa Azam anaitwa Leonel (Leonel Saint-Preux) kwa kuangalia video zake kwenye mtandao. Ni lazima klabu, na TFF zirudi kwenye azimio la Bagamoyo,”alisema Mayay

Azimio la Bagamoyo lilitiwa saini 2013 na mbali na kuweka idadi na viwango vinavyostahili kwa makocha wa kigeni, pia liliweka utaratibu wa klabu kuajiri watendaji mbalimbali.