Mashabiki wavunja mchezo dakika ya 88

Muktasari:

  • Mashabiki hao waliruka uzio kabla ya kufanya fujo uwanjani, vurugu ambazo zilimfanya mwamuzi kuumaliza mchezo huo zikiwa zimebaki dakika mbili mchezo kumalizika.
  • Tukio la kushitukiza la nyota wa Ivory Coast, Lamine Gassama la kuangushwa chini lilionyesha picha mbaya katika Uwanja wa Sebastien Charlety mjini Paris.

Paris, Ufaransa .Mchezo kati ya Ivory Coast na Senegal umelazimika kumalizika dakika ya 88 baada ya mchezaji kuvamiwa kwa mtindo wa rugby na mashabiki walioingia uwanjani na kuwasumbua wachezaji.

Mashabiki hao waliruka uzio kabla ya kufanya fujo uwanjani, vurugu ambazo zilimfanya mwamuzi kuumaliza mchezo huo zikiwa zimebaki dakika mbili mchezo kumalizika.

Tukio la kushitukiza la nyota wa Ivory Coast, Lamine Gassama la kuangushwa chini lilionyesha picha mbaya katika Uwanja wa Sebastien Charlety mjini Paris.

Mwamuzi Tony Chapron aliona dalili za hatari na kuamua kuwaondoa nyota hao wa kimataifa kwenda katika vyumba vya kubadilishia.

Tukio hilo la kuogopesha lilitokea wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki, ambao nyota wa Liverpool, Sadio Mane aliipa Senegal bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti.

Cyriac Gohi Bi aliisawazishia Ivory Coast dakika chache baadaye dakika ya 70.

Nyota wa Manchester United, Eric Bailly na winga wa Crystal Palace, Wilfried Zaha nao waliingia katika mzozo wakati wa mchezo huo.

Hii si mara ya kwanza kwa mechi kati ya timu hizo mbili za taifa kuwa na vurugu na kumalizika kabla ya muda wa kawaida, kwani miamba hiyo ya Afrika iliwahi kuahirishwa kwa mchezo wao 2012.