Maxime: Usajili wa dirisha dogo umelipa Kagera

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime

Muktasari:

Kagera hadi sasa imekusanya pointi 31, ikiwa nyuma ya virana wa Ligi Kuu Simba kwa pointi 13 na 12 nyuma ya Yanga inayoshika nafasi ya pili.

Dar es Salaam. Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema anajivunia usajili alioufanya katika kipindi cha dirisha dogo na anaamini kikosi chake kitaendelea kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara.

Kagera hadi sasa imekusanya pointi 31, ikiwa nyuma ya virana wa Ligi Kuu Simba kwa pointi 13 na 12 nyuma ya Yanga inayoshika nafasi ya pili.

Katika usajili wa dirisha dogo, Maxime aliwasajili kipa Juma Kaseja, Mohammed Fakhi na Ame Ally, wachezaji walioleta mabadiliko makubwa katika kikosi chake katika harakati za kusaka mafanikio msimu huu.

Maxime alisema anaamini kikosi chake kitaendelea kufanya vizuri licha ya presha iliyopo miongoni mwa timu shiriki.

“Ukijisahau umekwisha, tunatambua ligi ni ngumu hasa mzunguko huu wa pili, kila timu inataka matokeo na sisi hatutaki kupoteza. Tutajitahidi kushinda mechi za kutosha ili takae nafasi nzuri,” alisema Maxime. Alisema: “ ,”Unapokuwa kwenye nafasi nzuri, presha inapungua maana itafika wakati kuna timu zitakuwa zinalazimisha matokeo ili zisishuke daraja na nyingine zitwae ubingwa, tunajitahidi kuwa makini kwenye kila mchezo.”

Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili, Kagera imepoteza mchezo mmoja dhidi ya Mwadui, kushinda mechi mbili dhidi ya Stand United na Ndanda na kutoka suluhu dhidi ya Mbeya City