Mbao FC yapewa Sh150mil ijiendeshe

Mwenyekiti wa timu ya Mbao FC, Solly Njashi (kulia) akipokea jezi kutoka kwa mhasibu mkuu wa kampuni ya Hawaii, Said Khamis ikiwa ni mojawapo ya watadhamini timu hiyo kwa miezi sita. Makabidhiano yaliyofanyika katika ofisi za TFF jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Kampuni hiyo imetangaza kuipatia timu hiyo, Sh150 milioni kwa miezi sita ya mwisho ya Ligi Kuu Bara.

Dar es Salaam. Kama ilivyopata zali la kupanda Ligi Kuu, Mbao FC imepata zali la udhamini wa Kampuni ya Hawaii Product Supplies, watengenezaji na wasambazaji wa maziwa ya cowbell.

Kampuni hiyo imetangaza kuipatia timu hiyo, Sh150 milioni kwa miezi sita ya mwisho ya Ligi Kuu Bara.

Mbao ilipata zali la Ligi Kuu kwa mgongo wa Polisi Mara na Geita Gold ambazo zilishushwa daraja baada ya kubainika kujihusisha na vitendo vya upangaji wa matokeo.

Akizungumza jana wakati wa kuipatia udhamini timu hiyo, Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Elisalia Ndeta alisema wamewaongezea nguvu Mbao FC na watakuwa wakiwapa Sh25 milioni kwa mwezi kwa mkataba wa miezi sita.

Mbao FC, imepanda Ligi Kuu msimu huu ilianza kwa kusuasua kutokana na ukata na mzunguko wa pili itakuwa kwenye hali nzuri kutokana na udhamini huo.

Hadi kusimama kwa mzunguko wa kwanza, Mbao iko nafasi ya 12 ikiwa na ponti 16 na itaanza mzunguko wa kwanza

Ndeta alitoa sababu ya udhamini huo kwamba wamevutiwa na timu hiyo baada ya kufanya vizuri mechi za mwisho kwenye mzunguko wa kwanza.

Mhasibu mkuu wa kampuni hiyo, Ally Khamis alitiliana saini na uongozi wa timu hiyo katika Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mwenyekiti wa Mbao, Solly Zephania Njashi aliwashukuru wadhamini hao na kusema kwamba wamewapa nguvu na watawaongozea morali mzunguko wa pili.

“Imetutia moyo kwani timu ambazo zinalia ukata zipo nyingi hivyo kutuona sisi ni faraja na tutajipanga kuonyesha juhudi zetu,” alisema.

 

Mbao FC

Timu hiyo bado haipo katika sehemu salama kwani inaweza kushuka kama isipokuwa makini.

Ina changamoto kubwa ya safu ya ulinzi na tayari imeruhusu mabao 20 katika mzunguko wa kwanza hivyo anahitajika beki kuongeza nguvu na kupunguza uchochoro wa ngome.