Meneja wa Cheka uso kwa uso na Holyfield, Klitschko

Muktasari:

Kongamano hilo litafanyika kwa siku saba kuanzia Desemba 11 kwenye ukumbi wa Diplomat Beach, Resort and Spa in Hollywood uliopo Florida, Marekani.

Dar es Salaam. Meneja wa bondia Francis Cheka, Juma Ndambile na mabondia nguli duniani, Evander Holyfield na Vitali Klitschko wamekutana katika kongamano la kujadili maendeleo ya mchezo huo lililioandaliwa na Baraza la Ngumi la Dunia (WBC).

Kongamano hilo litafanyika kwa siku saba kuanzia Desemba 11 kwenye ukumbi wa Diplomat Beach, Resort and Spa in Hollywood uliopo Florida, Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na rais wa WBC, Mauricio Sulaiman, Ndambile amepewa nafasi hiyo kutokana na mchango wake katika kuwaendeleza na kuwasimamia mabondia wa ngumi za kulipwa nchini.

“Kongamano hili litawajumuisha wadau na mabondia wakubwa duniani kama Holyfield, Klitschko, Larry Holmes, Julio Cesar Chavez, Roy Jones Jr, Naseem Hamed na Eddie Mustapha,” alisema Sulaiman.

Wadau wengine wa ngumi watakaoshiriki ni Riddick Bowe, Terry Norris, Roberto Duran, Erik Morales, Marco Antonio Barrera, Milton McCrory, Montell Griffin na Vinnie Pazienza.

Kwa mujibu wa Sulaiman, katika hafla ya ufunguzi, wanatarajia kuwa na ‘First Lady’ wa ndondi, Lonnie Ali na wajumbe wengine kutoka kwenye familia ya mwanamasumbwi Muhammad Ali.

Akizungumzia nafasi aliyoipata, Ndambile alisema ni kubwa na kuahidi kuitumia kuitangaza Tanzania kwenye medani ya masumbwi kimataifa.

“Pia nitahakikisha natumia uzoefu na uwezo wa wenzetu kuendeleza zaidi mchezo huu hapa nchini kwani watu nitakaokutana nao katika kongamano hilo wana rekodi kubwa katika masumbwi duniani,” alisema Ndambile.