Msuva aondoka na matumaini kibao

Muktasari:

  • Msuva ameichezea Yanga kwa msimu minne, alisema kupata nafasi ya kucheza nchini humo ni mwanzo wa safari yake kuelekea kule anakokutamani hasa kucheza ligi kubwa duniani.

Dar es Salaam. Winga wa Yanga, Simon  Msuva aliondoka jana  kuelekea nchini Morocco kujiunga na klabu ya  Difaa Al Jadid huku  akidai kuwa huo ni mwanzo tu kwani malengo  yake ni kucheza Ligi Kubwa Ulaya hasa Ligi  Kuu Hispania.

Msuva ameichezea Yanga kwa msimu minne, alisema kupata nafasi ya kucheza nchini humo ni mwanzo wa safari yake kuelekea kule anakokutamani hasa kucheza ligi kubwa duniani.

Alisema atajituma kwa kiwango cha juu ili aweze kuzivutia timu mbalimbali za Ulaya na kufuata nyayo za Mbwana Samatta ambaye anaichezea  KRC Genk ya Ubelgiji.

"Kila mtu huwa ana malengo. Moja ya malengo yangu nilitamani kutoka kucheza nje ya nchi na sasa nimepeta nafasi hii hivyo nitahakikisha najituma na kuweza kutimiza malengo yangu mengine.

"Nitacheza huko kwa malengo  ya kwenda mbele zaidi kwani natamani siku moja nizheze moja ya ligi kubwa Ulaya  inagwa ninavutiwa ziadii na ligi ya Hispania"alisema Msuva. 

Msuva anaiacha Yanga baada ya msimu uliopita kuibuka mfungaji bora akiwa amefunga mabao 14 huku akiwa mmoja wa wachezaji waliochangia mabao wenzake ndani ya kikosi hicho.