Ndanda, Mingange kila moja amtupia lawama mwenzake katika usajili wa Ndanda

Muktasari:

  • Mingange kwa miaka miwili amefundisha timu mbili tofauti baada ya kufundisha timu za Mbeya City na Prisons zote za mkoani Mbeya na kisha amefundisha mara mbili Ndanda kabla ya msimu uliopita kwenda kuokoa jahazi timu hiyo isishuke.

Uongozi wa Klabu ya Ndanda upo katika sitofahamu ya kuendelea na kocha wao Meja mstaafu Abdul Mingange kuhusu kuendelea kukitumikia kikosi hicho ambacho kimenusurika kushuka katika msimu uliopita.

Mingange kwa miaka miwili amefundisha timu mbili tofauti baada ya kufundisha timu za Mbeya City na Prisons zote za mkoani Mbeya na kisha amefundisha mara mbili Ndanda kabla ya msimu uliopita kwenda kuokoa jahazi timu hiyo isishuke.

Mingange hadi sasa hajaanza pilika pilika za usajili kutokana na kutokufahamu hatima yake ndani ya kikosi hicho kutokana na uongozi huo kukaa kimya kwa muda bila kuwa na mawasiliano naye.

“Nipo kimya kwa sababu mimi niliitwa kwa muda mfupi kwenda kuipigania timu isishuke, sijajua sasa kama nitaendelea nao msimu ujao au vipi na ndio maana mnaona nipo kimya kwenye usajili lakini wakiniambia naanza usajili mara moja,”alisema Mingange.

Katibu mkuu wa Ndanda, Seleman Kachele alisema bado hawajaanza kusajili kutokana kuwa katika mazungumzo na kocha wao ambaye walikuwa naye kwa muda mfupi, lakini wakimalizana wataanza usajili wao.

“Usajili bado hatujaanza kwa sababu bado tupo katika mazungumzo na kocha, msimu uliopita tulikuwa naye kwa muda mfupi kwahiyo tunazungumza naye kwa kina tukikubaliana  ndipo tutaanza usajili wetu,”alisema Kachele.