Ndanda yajiandaa kushuka daraja

Dar es Salaam. Ndanda imejiweka katika  mazingira ya kufanya vibaya msimu ujao kutokana na wachezaji wengi wa kikosi hicho kutimkia. 

Mpaka sasa Ndanda ambayo msimu uliopita iliponea chupuchupu kushuka daraja haijafanya usajili wa maana  huku Ligi Kuu Bara msimu ujao ikiwa ni wiki tatu kabla ya kuanza.

Wachezaji saba wa kikosi cha kwanza wa Ndanda wametimkia timu nyingine akiwemo

nahodha Kiggi Makasy aliyehamia Singida United.

Wachezaji wengine walioondoka ni mshambuliaji  wao tegemeo, Riphat Hamis aliyejiunga na Mtibwa Sugar, kiungo Nassoro Kapama na beki Savatory Ntebe wako mbioni kujiunga na Majimaji pamoja na  beki Paul Ngalema na kiungo Willium Lucian 'Gallas' wanaotajwa kuhamia Lipuli ya Iringa.

Habari zinadai timu hiyo ilichukuliwa na mfadhili ambaye aliunda  safu mpya ya uongozi,  lakini fedha ndogo ya usajili waliyotaka kuwapa wachezaji wa kikosi hicho imegeuka kaa la moto kwani wengi waliamua kutimia.

Hata hivyo taarifa zaidi zinadai mfadhili huyo amemua  kuirejesha timu hiyo kwa uongozi wa zamani baada ya kuona suala la usajili kwa wachezaji limekuwa gumu.

Msemaji wa timu hiyo, Idrisa Bandari  alisema timu hiyo imenza mazoezi  masuala ya usajili  na wachezaji walioondoka hawezi kuyaweka wazi kwa sasa mpaka pale atakapopata ripoti kutoka uongozi wa juu.

"Timu imeshaanza mazoezi kujiandaa na ligi na ishu ya usajili siwezi kuisema kwa sasa  mpaka pale viongozi wa juu watakaponipatia ripoti kamili ndipo nitatangaza wachezaji tuliowasajili kwa ajili ya msimu ujao," alisema Bandari.

Hata hivyo, klabu hiyo iko katika mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Malimi Busungu.