Nduda aumia goti azua hofu Simba

Muktasari:

  • Kuumia kwa Ndunda ni pigo kwa Simba inayojiandaa na mchezo wake wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaofanyika Jumatano ijayo.

Kipa mpya wa Simba, Said Mohammed ‘Ndunda’amezua hofu katika kambi ya timu hiyo baada ya kuumia goti na kushindwa kumaliza mazoezi na wenzake jana jioni kwenye Uwanja wa Ngome uliopo Fuoni kisiwani Unguja.

Kuumia kwa Ndunda ni pigo kwa Simba inayojiandaa na mchezo wake wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaofanyika Jumatano ijayo.

"Nimeshtuka goti wakati wa mazoezi na nasikia maumivu, lakini daktari ameniambia kuwa siyo tatizo kubwa sana na litapona kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii," alisema kipa huyo.

Kama hali ya kipa huyo haitatengamaa, ni wazi kuwa  nafasi yake itazibwa na kipa namba tatu, Emmanuel Mseja  alisajiliwa kutoka Mbao FC.

Mbali ya Ndunda pia Simba kuna hatihati ya kumkosa nahodha wake msaidizi mshambuliaji John Bocco pamoja na beki Shomari Kapombe ambao bado hawajaanza mazoezi na wenzao kutokana na kusumbuliwa na majeruhi.