Nyamlani atangaza kujitoa kuwania urais TFF

Muktasari:

 

  • Nyamlani aliwasilisha barua TFF leo Jumapili, ikiwa ni siku moja tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais huku akieleza kwamba amefanya uamuzi huo kutokana na masuala binafsi.

Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani leo Jumapili ametangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais wa shirikisho hilo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12.

Nyamlani aliwasilisha barua TFF leo Jumapili, ikiwa ni siku moja tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais huku akieleza kwamba amefanya uamuzi huo kutokana na masuala binafsi.

Kwa msingi huo, wagombea wanaobaki kwenye kinyang’anyiro na kuhitajika kufika kwenye usaili kuanzia Juni 29, mwaka huu ni tisa wakiongozwa na Rais wa sasa, Jamal Malinzi anayetetea nafasi.

Mbali ya Malinzi wengine wanaowania nafasi hiyo ni Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.

Waliojitokeza kuwania Makamu wa Rais na kurejesha fomu wako Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.

Mbali ya nafasi za urais na makamu rais, Abdallah Mussa - aliyekuwa akiwania nafasi ya kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji TFF kutoka Kanda Na. 1 (Mikoa ya Kagera na Geita) aliondolewa kwa sababu ya kutoambatanisha kivuli cha cheti ya elimu ya sekondari.