Oden Mbaga: TFF imezima nyota yangu

Oden Mbaga

Muktasari:

  • Sasa ni miaka miwili tangu asimamishwe kuchezesha soka nchini.

Dar es Salaam. Mwamuzi Oden Mbaga amelitaja Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchangia kwa sehemu kubwa kuizima nyota yake ya uamuzi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Mbaga alisema TFF inapotosha ukweli kwa kuwasingizia Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kwamba ndiyo inahusika na kusimamishwa kwao.

Julai 24, 2014, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alitangaza kuwasimamisha Mbaga na wenzake Jesse Erasmo na Hamis Chang’walu kwa tuhuma za kupanga matokeo, ambazo hazikuwekwa wazi.

“Waamuzi hao waliosimamishwa na TFF pamoja na watu wengine watahojiwa na ujumbe huo wa Fifa na matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa na Fifa wenyewe baada ya uchunguzi huo kukamilika,” ilisema taarifa kutoka TFF kuelezea kufungiwa kwao.

Tangu kipindi hicho hadi sasa, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Fifa wala TFF juu ya uchunguzi huo, ambao ulifanyika. Mwamuzi huyo amefichua kuwa hakuna ukweli wa kile ambacho TFF wanakitaja kama sababu ya kusimamishwa kwake na badala yake kumetokana na majungu na fitina za watu wachache. Mbaga alisema.

“Machi 2014 zikazuka tuhuma kwangu, Mbaga amefoji matokeo, hakukimbia, kaandika kakimbia na jina lake limepelekwa Fifa, huyu lazima tumshtaki kwenye kamati ya maadili.”

“Bahati nzuri tulivyokwenda kwenye kamati ya maadili tumeitwa tukajieleza tukaonekana hatuna hatia kwamba kitu tulichokifanya ni kile tulichoelekezwa, hivyo kesi ile ilikosa mashiko mimi nikajua yamekwisha,” alisema Mbaga.

Alisema baada ya kuonekana hawana hatia, mmoja wa waamuzi wa soka nchini aliandika barua kwenda TFF kuwatuhumu kuwa wanajihusisha na rushwa.

“Sijui alitokea mwamuzi gani akaandika barua kwamba Mbaga, Erasmo na Chang’walu walikuwa wanatoa rushwa kwa Sunday Kayuni na Leslie Liunda ili waendelee kuwamo kwenye paneli ya Fifa na wana tuhuma nyingi.

“Kwa hiyo, hii ikawa ni sababu ya mimi kukaa nje kwamba hatukuwa waadilifu katika shughuli zetu za uchezeshaji, haijulikani ni mechi zipi, ni wapi na lini,” alisema Mbaga.

Mwamuzi huyo alisema aliamua kuzungumza na mwanasheria wake, Damas Ndumaro, ambaye alimshauri akate rufaa kwenda kamati ya maadili, ambayo hadi leo hii haijakaa kujadili suala lake.

Alisema kitendo cha TFF kuihusisha Fifa na kusimamishwa kwao siyo kweli na kinalenga kuzima suala hilo.

“Hakuna kusimamishwa na Fifa wala nini. Baada ya suala letu kutokea niliamua kuwasiliana na Fernando Tresaco, ambaye ni mkuu wa idara ya waamuzi wa Fifa. Alitujibu kwamba kweli alipokea suala letu, ambaye alitujibu kuwa kama hatujapata barua yoyote Fifa basi linaonekana halina mashiko,” alisema Mbaga. Alisema muda wote amekuwa akiwasiliana na Fifa, lakini jibu wanalompa ni kuwa wao hawaoni kosa ambalo Mbaga na wenzake wamefanya.

Mbaga alisema kuwa Fifa ilimwambia kuwa wanaoweza kulimaliza suala lake ni TFF ambao nao wanaonekana kuutupa mpira huo kwa Fifa.

 

Usikose mwendelezo wa mkasa wa mwamuzi Mbaga kesho.