Okwi ataka taji Ligi Kuu Uganda

Muktasari:

  • Pamoja na kukiri kuwa ubingwa utakuwa mgumu kwa kwao kwa sababu  ya kutegemea matokeo ya wapinzani wao,  lakini Okwi amesisitiza kwamba hawawezi kurudi nyuma kwa sababu kimahesabu jambo hilo linawezekana.

Kampala, Uganda. Wakati Ligi Kuu Uganda ikielekea mwishoni, mshambuliaji wa SC Villa, Emmanuel Okwi amekiri wanatakikuwa kufanya kazi ya ziada kupata ubingwa msimu huu.
Pamoja na kukiri kuwa ubingwa utakuwa mgumu kwa kwao kwa sababu  ya kutegemea matokeo ya wapinzani wao,  lakini Okwi amesisitiza kwamba hawawezi kurudi nyuma kwa sababu kimahesabu jambo hilo linawezekana.
SC Villa ipo nafasi ya pili wakitofautiana kwa mabao na vinara KCCA baada ya timu hizo kutoka sare 1-1 mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na mtandao wa Kawowo Sports, Okwi alisema walicheza vizuri na kumiliki mpira hata hivyo bahati haikuwa kwao.
“Sasa ni dhahiri ubingwa haupo mikono mwetu, lakini bado kimahesabu tunayo nafasi ya kushinda taji msimu huu.”
“Sitaki kuzungumza sana, lakini ni dhahiri hatukuwa na bahati na mwishowe tulipata sare. Tunatarajia kushinda michezo mingine inayofuata.”
Okwi alisawazishia Villa kwa bao la shuti la umbali wa mita 12 na kufuata bao la awali la KCCA lililofungwa na Geofrey Sserunkuma.
Villa sasa italazimika kuomba dua baya kwa KCCA ilipoteza mechi zake zilizosalia na wenyewe kushinda mechi zilizosalia ili kujihakikishia kutwaa ubingwa msimu huu.