Pluijm kufumua kikosi Yanga

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm 

Muktasari:

Kauli hiyo ilitolewa jana baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United katika mchezo ambao Yanga imepoteza kwa mara ya kwanza msimu huu.

Shinyanga. Kama alivyobashiri kabla ya kuondoka Dar es Salaam kwenda Shinyanga kuwa mechi za huko zitakuwa ngumu kwao, kocha wa Yanga, Hans Pluijm amepania kufumua kikosi chake ili kutengeneza imara kuikabili Simba katika mchezo wa watani wa jadi, Jumamosi wiki hii.

Kauli hiyo ilitolewa jana baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United katika mchezo ambao Yanga imepoteza kwa mara ya kwanza msimu huu.

Akizungumza baada ya kushuhudia timu yake ikipokea kipigo hicho kwenye Uwanja wa Kambarage, kocha Pluijm alisema matokeo hayo yalitokana na mabeki wake kukosa uelewano na kusababisha wapinzani wao kufunga bao hilo.

“Kutakuwa na mabadiliko makubwa katika mchezo ujao dhidi ya Simba, nataka kutengeneza kikosi imara, hivyo nitabadilisha wachezaji wengi katika mechi inayokuja,” alisema Pluijm kwa ufupi bila ya kufafanua ni mabadiliko yapi atakayofanya kwenye kikosi chake Jumamosi.

Safu ya ulinzi ya Yanga jana ilianza na kipa, Ally Mustapha ‘Barthez’, akisaidiwa na mabeki Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vincent Bossou, Andrew Vincent, hivyo mabadiliko hayo yatafungua milango kwa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub kurejea kwenye kikosi ambacho kitaivaa Simba.

Baadhi ya mashabiki wa Yanga walifanya vurugu uwanjani hapo (Kambarage) baada ya filimbi ya mwisho wakiwalaumu viongozi wao kwa kushindwa kufuata masharti ya kuingia uwanjani kwa kutumia lango dogo badala yake wameingilia lile kubwa.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, wameonja adha ya kufungwa katika ligi msimu huu wakati wakijiandaa na mchezo dhidi ya watani zao wa jadi, Simba Jumamosi.

Mshambuliaji Pastory Athanas alifungia Stand United bao pekee katika dakika 58 ya mchezo baada ya kupokea pasi ndefu kutoka katikati ya uwanja wa kumzidi mbio Haji Mwinyi na kupiga shuti la chini lililomshinda kipa Ally Mustapha na kujaa wavuni.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuporomoka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 10, sita nyuma ya Simba wanaoongoza ligi hiyo wakati Stand United yenye migogoro nje ya uwanja ikipanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 12, wakati Azam waliokubali kipigo cha mabao 2-1 juiz kutoka kwa Ndanda FC ya Mtwara wameshuka hadi nafasi ya nne.

Wakicheza mbele ya mashabiki wao, Stand waliuanza mchezo huo kwa kasi na kulishambulia lango la Yanga dakika ya 12, mkongwe Adam Kingwandwe alikosa bao baada ya kupokea pasi ya Kelvin Sabato.

Yanga ilijibu mapigo kupitia washambuliaji wake, Donald Ngoma na Amissi Tambwe, lakini mashuti yao yalishindwa kulenga lango la Stand United katika dakika 19 na 22.

Kipindi cha pili Stand United iliingia kwa kasi zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza na dakika 58, Athanas alifunga bao kwa shuti la chini lililomshinda kipa Barthez na kujaa wavuni.

Mshambuliaji Ngoma alinusurika kupewa kadi nyekundu baada ya kumkwatua kwa nyuma beki wa Stand United, Adeiyum Saleh, lakini mwamuzi Ngole Mwangole alimuonyesha kadi ya njano.

Kocha wa Stand, Mfaransa Patrick Liewig aliwapumzisha Geremy Katula nafasi yake kuchukuliwa na Frank Khamis wakati kocha Pluijm alimtoa Ngoma, Deus Kaseke na kuwaingiza Obrey Chirwa na Juma Mahadhi.

Mabadiliko hayo hayakuwa na faida kwa Yanga iliyoendelea kucheza bila ya malengo uwanjani huku Stand United ikimarika zaidi katika safu ya ulinzi.

Kiungo Mahadhi alisema ni matokeo mabaya kwao, hawakuyatarajia, lakini ndiyo mpira unavyokwenda na wao wanakwenda kujipanga kwa mchezo ujao.

Katika michezo mingine Ruvu Shooting ililazimishwa sare 0-0 na Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza, Coastal Union imenyukwa mabao 2-1 na Polisi Morogoro.

 

Vikosi vilivyocheza

Stand United: Frank Muwonge, Revocatus Richard, Adeyum Saleh, Erick Mulilo, Ibrahim Job, Jacob Masawe, Pastory Athanas, Geremy Katura, Kelvin Sabato, Seleman Kassim ‘Selembe’ na Adam Kingwande.

Yanga:Ally Mustapha, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vincent Bossou, Vincent Andrew, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.