Polisi yapania kuipoka ubingwa Uhamiaji

Muktasari:

  •  Uhamiaji ni bingwa mara tatu wa mashindano hayo yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Sheik Amri Abeid, ambapo mkoa wa Arusha utawakilishwa na timu tatu za Polisi, Madini na Arusha City Queens.

Arusha. Timu ya netiboli ya Polisi imejinga kuivua ubingwa Uhamiaji wakati wa mashindano ya kusaka klabu bingwa ya Tanzania Bara yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 13 mwaka huu jijini Arusha.

 Uhamiaji ni bingwa mara tatu wa mashindano hayo yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Sheik Amri Abeid, ambapo mkoa wa Arusha utawakilishwa na timu tatu za Polisi, Madini na Arusha City Queens.

 Kocha wa Polisi Arusha, Emerciana Silas alisema nafasi ya wenyeji waliyopewa wataitumia vizuri kuhakikisha ubingwa unabaki hapo ili kuonyesha klabu zingine za mikoani kutoa fikra kuwa kombe hili si la mkoa wa Dar es Salaam

 “Mwaka huu sisi ndio wenyeji na tunataka kuonyesha wenyeji wetu kwa timu tutakazochuana nazo kuwa tuko nyumbani na hao walioshikilia kombe miaka yote wajiandae kuliachia.”

  “Niseme tu kuwa kimazoezi tuko vizuri na tunafanya hapa hapa, hivyo kwa mwaka huu hakuna jipya chini ya jua tutakalolishindwa na uzuri mbinu zao (Uhamiaji) hivyo kikubwa kwa sasa wadau wa Arusha waje washuhudie tunavyochukua kombe,” alisema Silas.

 Mwenyekiti wa Chaneta, Anna Kibira alisema wameamua kuyaleta mashindano hayo mkoa wa Arusha ili kutoa fursa kwa timu wenyeji kujaribu bahati yao ya kupoka ubingwa wa uhamiaji.

 “Arusha ndio ina timu nyingi na misimu ya hivi karibuni wameonekana kuamka sana hivyo tukaona ni bora na wao kuwapa nafasi ya wenyeji ili kuzidisha amsha amsha ya mchezo huo zaidi na kujaribu bahati yao.”