Prisons yajichimbia Zanzibar, kunoa makali Ligi Kuu

Muktasari:

  •  Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza inakuwa timu ya tatu kuweka kambi visiwani humo baada ya  Simba na Yanga  zinazojiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii.

Dar es Salaam. Tanzania Prisons imeweka kambi Visiwani Zanzibar  kujiandaa na Ligi Kuu Bara itakayoanza Agosti 26.

 Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza inakuwa timu ya tatu kuweka kambi visiwani humo baada ya  Simba na Yanga  zinazojiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii.

Katibu Mkuu wa Prisons, Havinitishi Abdallah alisema wamuamua kweka kambi visiwani humo kutokana na hali ya hewa ya visiwa hivyo na utulivu uliopo.

“Tuna siku nne tangu tumefika hapa na watu wasitushangae kwa sababu si mara ya kwanza kuja hapa na haitakuwa mara ya mwisho. Tutaendelea kuja kadri ya mipango yetu,”alisema Abdallah aliyekabidhiwa mikoba ya ukatibu mkuu kutoka kwa Osward Morris.

Maandalizi hayo pia yanajumuisha kikosi cha vijana chini ya miaka 20 ambacho pia kinajiandaa na ligi ya vijana.

“Hata timu ya vijana ipo na juzi ilicheza mechi ya kujipima nguvu na KMKM na kesho itacheza na Mlandege, msimu huu tumejipanga kufanya vizuri,”alisema

Beki, Salum Kimenya alisema amedhamiria kulinda mafanikio ya msimu uliopita na ikiwezekana kushinda tuzo ya mchezaji bora.

“Ni kazi kulinda mafanikio, ndio maana napambana. Bado nina muda mrefu wa kucheza. Lengo langu ni kuendeleza nilipoishia,”alisema Kimenya ambaye nusura atue Azam kwenye dirisha la usajili lililomalizika Agosti 6.

Prisons itaanza kampeni ya kuwania taji la Ligi Kuu, Agosti 26 kwa kucheza na Njombe Mji kwenye Uwanja wa Sabasaba uliopo Mkoani Njombe.