Rais wa Fifa kuibeba Afrika WC

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino.

Muktasari:

  • Wakati wa kampeni zake kabla ya kuingia madarakani Februari mwaka huu, raia huyo wa Uswisi mwenye asili ya Italia alieleza dhamira yake ya kuhakikisha fainali za Kombe la Dunia (WC) mwaka 2026 zinakuwa na timu 40 badala ya 32 za sasa.
  • Akiwa ziarani Nigeria, bosi huyo wa Fifa alieleza kuwa ndoto yake itatimia na Afrika ni bara litakalonufaishwa na ongezeko hilo.

Abuja, Nigeria. Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino ameendeleza  sera zake za kutaka fainali za Kombe la Dunia miaka kumi ijayo ziwe na timu 40, zikiwamo saba kutoka Afrika.

Wakati wa kampeni zake kabla ya kuingia madarakani Februari mwaka huu, raia huyo wa Uswisi mwenye asili ya Italia alieleza dhamira yake ya kuhakikisha fainali za Kombe la Dunia (WC) mwaka 2026 zinakuwa na timu 40 badala ya 32 za sasa.

Akiwa ziarani Nigeria, bosi huyo wa Fifa alieleza kuwa ndoto yake itatimia na Afrika ni bara litakalonufaishwa na ongezeko hilo.

Alieleza matumaini ya kubadili pia mfumo wa kufuzu kwa timu zinazoshiriki fainali hizo, akieleza matumaini ya kuipa Afrika nafasi mbili kutoka tano za sasa.

Alieleza mabadiliko hayo wakati akimtambulisha beki wa zamani wa Nigeria, Joseph Yobo kuwa balozi wa heshima wa ligi wa nchi hiyo (NPL).

Hata hivyo, Infantino atalazimika kupigana kiume ili kuhakikisha pendekezo lake linapitishwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo.