Real yamletea makali Benzema

Muktasari:

Benzema amejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza Real Madrid lakini hajaitwa kwenye kikosi cha Ufaransa tangu mwaka 2015 kutokana na kuwa na mashtaka polisi baada ya kudukua taarifa za mchezaji mwenzake wa kimataifa Mathieu Valbuena.

Madrid, Hispania. Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amesema kwamba anaamini kwamba Karim Benzema ndiye mcheaji bora namba tisa duniani na anafikiria kumuongezea nguvu kwa kumleta kikosini Kylian Mbappe.
Benzema amejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza Real Madrid lakini hajaitwa kwenye kikosi cha Ufaransa tangu mwaka 2015 kutokana na kuwa na mashtaka polisi baada ya kudukua taarifa za mchezaji mwenzake wa kimataifa Mathieu Valbuena.
Mchezaji huyo mwenye miaka 29 amekanusha mashtaka yote yanayomkabili na keshi hiyo bado haijafikishwa mahakamani.
Hata hivyo, Rais wa Madrid amemzungumzia kiungo huyo kama mchezaji bora Mfaransa na anatarajia kuona akimaliza maisha yake soka akiwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu.
“Benzema ni mchanganyiko wa wachezaji wawili ambayo ni Zinedine Zidane na Christiano Ronaldo,” Perez aliliambia gazeti la RMC, huku akisisitiza kwamba huyo ndiye mchezaji bora namba tisa kwa sasa duniani.
“Ninashawishika kwamba ataendelea kuwapo Real Madrid, kwa sasa hatujaanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba wake ingekuwa ni uwezo wangu ningemwacha acheze hapa kwa kipindi chake chote cha maisha yake ya soka.”
“Ninafurahia kuona uwepo wa Benzema pia ni mtu mwenye tabia njema.”
Mbappe amekuwa mchezaji huru baada ya kumalizana na Monaco jambo linalompa nafasi kubwa  kwenda klabu yoyote katika kipindi cha msimu wa dirisha la usajili.
Wakati Perez akisema hawezi kuzungumzia iwapo kuna uwezekanao wa kumchukua Mbappe kwenye kikosi cha Madrid, laikini alikuwa na nia ya kumuongezea nguvu Benzema kwa kumsajili kijana huyo wa miaka 18.
“Muunganiko wa Benzema na Mbappe? Kila kitu kinawezekana,” aliongeza
“Lakini katika kipindi cha msimu huu, sitaki kuzungumzia kuhusu wachezaji wa timu nyingine. Kwa sasa tunafikiria ni namna gani tutashinda taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.”