Monday, June 19, 2017

Samatta: Nikiondoka Genk nakwenda England, Hispania au Italia

 

By Majuto Omary

 Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta  amesema  amepokea ofa mbalimbali za kucheza soka la kulipwa katika klabu za Ligi Kuu za England, Hispania, Ujerumani na Italia.

Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji katika klabu ya KRC Genk amesema kuwa hiyo ni faraja kwake na kwa sasa wakala  na viongozi wa klabu ya Genk wanashughulikia suala hilo na hatma yake itajulikana baadaye.

Amesema kuwa kutokana na masharti ya mkataba, hataweza kuzitaja klabu hizo mpaka makubaliano baina ya klabu hizo, wakala wake na viongozi wa timu ya Genk.

“Ni faraja kwangu kupokea ofa hizo, ni muhimu katika maendeleo yangu ya soka, naona mwanga na naamini ndoto yangu ya kucheza soka la kulipwa katika nchi hizo zitatimia,” alisema Samata ambaye kwa sasa ni balozi wa benki ya DTB.

Amefafanua kuwa klabu nyingi ni za daraja kati na mazungumzo yanaendelea vizuri. Amesema kuwa nia yake kubwa ni kucheza nje ya Ubelgiji kwa makubaliano ambayo yatawaridhisha viongozi wake wa klabu ya Genk.

“Ofa zangu ni za klabu ambazo hazipo chini katika msimamo, wala juu ya msimamo, ni vya katikati, ni fursa hiyo, hivyo wakala wangu na viongozi wa timu wakikubaliana na ofa zilizopo, nitakuwa tayari kuweka wazi,” alisema.

Amesema kuwa hataki kuonekana mchezaji mwenye matatizo katika masuala ya usajili na faraja kubwa kwake ni kuona kila upande unaridhika kutokana na makubaliano yatakayofikiwa.

Samatta amesema bado anamkataba wa miaka mitatu zaidi na timu ya Genk na anafurahia maisha ya nchi hiyo kutokana na ushirikiano mkubwa anaoupata.

-->