Samatta amtisha kocha wa Botswana

Muktasari:

  • Samatta aliwaadhibu Botswana kwa kufunga  bao la kwanza dakika ya pili, baadaye kufunga la pili kwa shuti la adhabu kiufundi dakika ya 87, pia alionekana kuwa hatari kwenye lango la Botswana mara kadhaa.

Dar es Salaam. Kocha wa Botswana, Peter Butler ameukubali uwezo wa mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta aliyepachika mabao mawili kwenye mchezo wa kirafiki, ambao ulichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Samatta aliwaadhibu Botswana kwa kufunga  bao la kwanza dakika ya pili, baadaye kufunga la pili kwa shuti la adhabu kiufundi dakika ya 87, pia alionekana kuwa hatari kwenye lango la Botswana mara kadhaa.

Utofauti wa matokeo umetajwa kusababishwa na Mshambuliaji huyo wa KRC Genk ya Ubelgiji kutokana na uwezo wake mzuri wa kucheka na nyavu alionao, licha ya muda mwingi Botswana kuoneka kumiliki asilimia kubwa ya mchezo.

"Ni ngumu kucheza ugenini kwa huku Afrika, lakini timu yangu imejitahidi kucheza vizuri, muda mwingi tulikuwa tunamiliki mpira lakini haikutusaidia pamoja na kuwa tulibadili mfumo kwa lengo la kutaka tutengeneze nafasi.

"Nahodha wa Tanzania 'Samatta' alicheza vizuri na ndiye aliyekuwa mchezaji hatari zaidi kwetu kipindi chote cha mchezo, amefunga mabao mawili ambayo yameleta utofauti, kwa kipindi chote Tanzania walikuwa bora kwenye eneo lao la ushambuliaji ukilinganisha na timu yangu.

"Tumepata ushindani wa kutosha kitu ambacho nilikuwa nakihitaji kwenye timu yangu, ambayo imeundwa na vijana nadhani hata kwa Tanzania itakuwa hivyo kwakuwa tumewapa upinzani, bila shaka kocha naye atakuwa ameufurahia upinzani tulioutoa kwa timu yake," alisema Butler.

Kocha huyo wa Botswana aliwai kuzitumikia klabu ya West Bromwich Albion mwaka 1992–1994 ambapo alicheza mechi 70 na kufunga mabao 3 akitumika kama kiungo  na baadaye alitua Notts County ambako hakudumu kwa misimu mingi na mwishowe alisajiliwa West Ham United zote za nchini Uingereza.

Kipa wa Botwana, ambaye alitunguliwa mabao mawili na Samatta, Kabelo Dambe anayekipiga kwenye klabu ya Platinum Stars nchini Afrika Kusini alisema mshambuliaji huyo ni moja katiwashambuliaji bora Afrika, ambao amekumbana nao.

"Amenifunga mabao ambayo si mepesi, lile la kwanza ilikuwa nilisogea kidogo ili kulifanya goli kuwa dogo kwa mshambuliaji, lakini alinifunga kwenye hali ile na hata bao la pili alitumia akili kwasababu niliwapanga wachezaji wenzangu kwenye ukuta.

"Alichokifanya nahodha wa Tanzania ni kupiga mpira kwa haraka kabla ya hata sijakaa sawa golini, lakini tulijitahidi kucheza vizuri ila hatukuwa na bahati ya kufunga mabao kitu ambacho wenzetu waliweza," alisema Dambe.