Samatta kuitega Stars kufuzu CHAN

Mshambuliaji Mbwana Samatta

Muktasari:

Stars itacheza na Burundi ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya kuwania kufuzu fainali za CHAN  2018 zitakazofanyika Kenya, huku Tanzania ikipangwa na Rwanda na mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam Julai 14 na marudiano Julai 21.

Dar es Salaam. Wakati Taifa Stars ikishuka kuivaa Burundi leo katika mchezo kirafiki, wadau soka nchini wamesema utegemezi wa mshambuliaji Mbwana Samatta huenda ukaigharimu timu hiyo katika mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani CHAN 2018.
Stars itacheza na Burundi ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya kuwania kufuzu fainali za CHAN  2018 zitakazofanyika Kenya, huku Tanzania ikipangwa na Rwanda na mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam Julai 14 na marudiano Julai 21.
Tanzania tangu ilifuzu CHAN 2009, Ivory Coast imeshindwa kufuzu kutokana na ubutu wa safu ya ushambuliaji wa ndani.
Kutokana na ubutu wa washambuliaji wa ndani imewalazimu makocha wa Stars kumtegemea Samatta anayechezea KRC Genk kama mkombozi kwenye mashindano ya kimataifa.
Makali ya Taifa Stars kwa asilimia kubwa yamekuwa yakichagizwa na ubora wa Samatta na pindi mshambuliaji huyo anaposhindwa kufurukuta, Stars imekuwa ikipwaya mara kwa mara.
Utegemezi huo wa Stars kwa Samatta ulianza tangu akiwa na TP Mazembe kabla ya kusajiliwa na Genk mwanzoni mwa mwaka jana.
Kuanzia mwaka 2011 hadi sasa,  Samatta ameifungia Stars mabao 17 katika mechi 39 alizoichezea,  idadi ambayo haijaweza kufikiwa na mchezaji yeyote wa Kitanzania kwenye timu ya taifa.
Kudhihirisha hilo,  tangu mwaka 2011 hadi sasa, hakuna mshambuliaji mwingine aliyeifungia Stars mabao angalau nusu ya mabao ya Samatta.
Hali hiyo ya kumtegemea zaidi Samatta huenda ikaipa wakati mgumu Stars  itakaposhiriki mashindano ya CHAN.
Hofu hiyo tayari imeshaanza kuonyeshwa na mshambuliaji wa Kagera Sugar,  Mbaraka Yusuph ambaye amekiri kumkosa Samatta itakuwa pigo kwa Stars kwenye mashindano ya CHAN.
“Ni kiongozi wetu na ukitazama kwenye kikosi chetu, yeye ndiye mchezaji aliyepiga hatua kubwa zaidi na kupata mafanikio mengi kisoka kulinganisha na wengine.
Wakati huo huo, nahodha wa Burundi, Rashid Hererimana amesema watautumia mchezo wa leo kama sehemu ya maandalizi ya mechi za kuwania kufuzu Fainali za Afrika. Aliwataka mashabiki kushuhudia mchezo huo akiamini utakuwa wa ushindani.
Ratiba
Tanzania v Burundi (10:00 jioni).