Sunday, January 8, 2017

Siku 113 ngumu za lala salama Ligi Kuu

By Fredrick Nwaka, Mwananchi fnwaka@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu Tanzania ikitarajiwa kuendelea Januari 13 ni dhahiri kuwa hatua  hiyo itakuwa ngumu, kuvutia na kuumiza baadhi ya timu.

Ligi hiyo imesimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea Zanzibar ambayo itafikia kikomo Januari 13 na Ligi Kuu itaanza Januari 13, 14, 15 na 16 kwa michezo ya raundi ya 19 kuchezwa.

Baada ya Ligi Kuu kuingia mzunguko wa 19, hakutakuwa na mapumziko ya mara kwa mara, bali pale Azam na Yanga zitakapokuwa zinacheza mechi za kimataifa na kutakapokuwa na mechi za Kombe la Shirikisho (ASFC).

JKT Ruvu itacheza na Ruvu Shooting Januari 13, Januari 14 kutakuwa na michezo miwili, Stand United itapepetana na Mwadui na Kagera Sugar itacheza na Ndanda FC. Januari 16, Simba itakuwa mgeni wa Mtibwa mkoani Morogoro, Majimaji ikiikaribisha Yanga mjini Songea na Azam itakuwa Azam Complex kucheza na Mbeya City.

Kimbembe cha ugumu wa ligi hiyo kinachangiwa na takwimu ambazo hadi sasa zinaonyesha Simba ikiwa kileleni na pointi 44, ikiwa ni pointi nne zaidi ya Yanga yenye pointi 40.

Hata hivyo, Majimaji, Toto Africans na JKT Ruvu hazina budi kuhakikisha zinashinda mechi zinazofuata ili kujiepusha na mkasa wa kushuka daraja.

Ruvu JKT inashika mkia ikiwa na pointi 14, Toto iko nafasi ya 15 ikiwa na pointi 16 na Majimaji ina pointi 17 na iko nafasi ya 14. Kwa mujibu wa ratiba, ligi hiyo itafikia tamati Mei 6, mwaka huu.

-->