Simba ukuta, Yanga mabao

Muktasari:

Timu hizo mbili zipo kwenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu

Dar es Salaam. Simba inapaswa kuishukuru safu yake ya ulinzi vinginevyo hivi sasa ingekuwa msindikizaji tu katika vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati Yanga sehemu kubwa inabebwa na washambuliaji wenye uchu wa kufumania nyavu.

Safu hiyo ya ulinzi ya Simba, imefanya kazi ya ziada kulinda ushindi kiduchu pamoja na matokeo ya bila kufungana kwenye baadhi ya mechi za Ligi Kuu, ambazo iwapo mambo yangekuwa kinyume, timu hiyo leo ingekuwa inalia na kusaga meno.

Ngome ya Simba

Kazi ya kwanza kubwa iliyofanywa na ukuta wa Simba ni kuilinda timu hiyo pointi tatu ilizopata kwenye mechi tatu ilizotoka sare dhidi ya Yanga, Mtibwa Sugar na JKT Ruvu msimu huu.

Iwapo mabeki wa Simba yenye pointi 45 sasa wasingezilinda pointi hizo tatu, leo hii ingekuwa pointi sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 43.

Ukuta huo wa Simba, ambao umeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita hadi sasa, ungeweza kuiweka pabaya zaidi timu hiyo iwapo ungeshindwa kulinda ushindi kiduchu wa bao 1-0, ambao Simba imeupata kwenye mechi tano msimu huu dhidi ya Azam FC, Mbao FC, Stand United, JKT Ruvu na Ruvu Shooting.

Iwapo timu hizo zingefanikiwa kupata bao moja tu la kusawazisha kwenye mechi hizo, ina maana kuwa Simba ingepoteza pointi 10, ambazo zingeifanya leo iwe nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi nane.

Hii inadhihirisha kuwa safu ya ulinzi ya Simba imefanya kazi kubwa msimu huu kulinganisha na ile ya ushambuliaji, ambayo imekuwa ikiiangusha timu hiyo.

Kwa wastani, Simba inaruhusu bao moja kila baada ya mechi tatu, wakati safu yao ya ushambuliaji ikifunga wastani wa bao 1.6 katika kila mechi inayocheza.

Takwimu hizo zinaashiria kuwa washambuliaji wa Simba hawatimizi ipasavyo majukumu yao ndani ya timu hiyo tofauti na safu yao ya ulinzi, ambayo imekuwa nguzo imara kwa mafanikio ya Simba msimu huu.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alifichua kuwa jambo kubwa linalotofautisha safu ya ulinzi na ushambuliaji ni umakini kwa wachezaji wanaocheza nafasi hizo.

“Washambuliaji wakiongeza umakini ambao wanaukosa pindi tunapokuwa tunashambulia, nina uhakika tutafunga mabao mengi. Sina shaka na safu yetu ya ulinzi kwa sababu inafanya vile ambavyo benchi la ufundi huwa linawaelekeza na ndiyo maana tumekuwa timu ambayo haijaruhusu mabao mengi hadi sasa,” alisema Mayanja.

Kiungo wa timu hiyo, James Kotei alisema hali kama hiyo ni ya kawaida kutokea kwenye timu ingawa ni lazima ifanyiwe kazi ili timu iweze kupata matokeo mazuri.

“Timu inacheza vizuri, lakini ni lazima ipate matokeo ili yaendane na kiwango cha uwanjani. Hii ni changamoto ambayo tunapaswa kuipokea na kuifanyia kazi ili tuweze kutimiza lengo la kutwaa ubingwa. Muda bado upo,” alisema Kotei.

Yanga wanafunga tu

Wakati mwingine inashangaza. lakini ndiyo ukweli kuwa Yanga haishikiki katika suala la upachikaji mabao kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

Sasa sikia hii, Yanga peke yake imefunga mabao mengi zaidi ya mabao yote yaliyofungwa na timu tatu zinazoshika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu.

Hata hivyo, kingine kinachovutia ni kwamba mabao yote waliyofunga vinara wa ligi, Simba ukichanganya na mabao yote ya vibonde wa ligi JKT Ruvu, hayafikii

40 ya Yanga waliyofunga kwenye ligi.

Hadi sasa, Yanga imefunga mabao hayo

, wakati timu tatu zilizoko mkiani kwenye msimamo wa ligi ambazo ni JKT Ruvu, Toto Africans na Majimaji kwa ujumla wao zimefunga mabao 32 tu.

Majimaji iliyo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi imefunga mabao 13, wakati Toto African ina mabao 12 na JKT Ruvu ikifunga mabao saba, hivyo kufanya timu zote tatu hadi sasa kufunga mabao 32, mabao manane pungufu kwa Yanga.

Pia, ukichanganya mabao ya timu tatu nyingine, Prisons, Mwadui na African Lyon bado hayawezi kuyafikia mabao 40 ya Yanga.

Mwadui imefunga mabao 16, wakati Prisons na African Lyon zimefunga mabao 11 kila moja na hivyo jumla zote kufunga mabao 38.

Achana na vibonde, ukiangalia timu za juu. Mabao 40 ya Yanga yameifanya kuwazidi vinara Simba kwa mabao 10, huku wakiizidi Kagera Sugar iliyoko katika nafasi ya tatu kwa mabao 19. Kagera imefunga mabao 21.

Ukichukua mabao 30 ya vinara wa ligi, Simba na saba ya wanaoshika mkia, JKT Ruvu Jumla ni mabao 37, ambayo hayafiki mabao 40 ya Yanga