Simba vs Yanga: Ni mchezo wa namba

Kumekucha uwanja wa taifa, Simba Yanga watambiana

Muktasari:

  • Zifuatazo ni namba zinazohusiana na mpambano wa leo.

>> Simba yapata bao dk 66, Mavugo amefunga akiunganisha pasi ya Kichuya

Simba yapata bao dk 66, Mavugo amefunga akiunganisha pasi ya Kichuya

Kipindi cha pili kimeanza, beki wa simba Besala Bokungu amepewa kadi nyekudu


Mpira ni mapumziko, Yanga wakiwa wanaongoza kwa bao moja dhidi ya Simba


Simba imepata faulo mbili karibu na goli lakini imeshindwa kutumia vizuri

Yanga inaongoza kwa bao moja, imepata kwa njia ya penalti dakika ya 6 lililofungwa na Simon Msuva

Dar es Salaam. Ilikuwa wiki ya kelele, tambo, majivuno na sasa, yamatimia. Leo ni leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba inacheza na Yanga mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Mechi ya kwanza Oktoba Mosi, timu hizo zilifungana bao 1-1.

Zifuatazo ni namba zinazohusiana na mpambano wa leo.

90: Dakika zitakazotoa mshindi wa leo, vinginevyo ni sare.

83 :Idadi ya michezo ya ligi ambayo Simba na Yanga zimekutana tangu 1965, ambao mfumo wa Ligi Kuu ulianza kutumika rasmi nchini.

04: Simba imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara tangu msimu wa 2011/2012.

14: Nyota wa kigeni wanaozitumikia Simba na Yanga. Yanga ina Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Vincent Bossou, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa, Justine Zulu na Amissi Tambwe. Simba ni Method Mwanjali, Juuko Murshid, Daniel Agyei, James Kotei, Janvier Bokungu na Laudit Mavugo.

17: Mabao ambayo timu zote mbili zimefungwa hadi sasa katika ligi. Yanga imeruhusu mabao tisa, wakati Simba wakifungwa nane.

 

82: Jumla ya mabao ambayo timu zote mbili zimeyafunga kwenye Ligi Kuu msimu huu. Simba mabao 36 wakati Yanga 46.

53: Umri wa kocha wa Yanga, George Lwandamina.

45: Umri wa kocha wa Simba, Joseph Omog.

26: Idadi ya vikombe vya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo Yanga imetwaa tangu ilipoanzishwa 1935.

18: Simba imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 18 tangu ilipoanzishwa 1936.

7: Tangu 1965, Simba na Yanga zimekutana mara saba katika Februari, kati ya hizo, Simba imeshinda mara moja wakati Yanga imeibuka na ushindi mara nne, huku wakitoka sare mara mbili.

170: Katika mechi 82 ambazo timu hizo mbili kongwe zimekutana kwenye Ligi Kuu kuanzia 1965, mabao 170 yamefungwa, Yanga ikifunga 92, wakati Simba 78.

6: Mchezaji wa zamani wa Yanga, Omary Hussein 'Keegan' anaongoza kuifunga Simba mabao mengi katika mechi za Simba na Yanga, akifunga mabao sita.

27: Namba ya jezi ya mshambuliaji Saimon Msuva, ambaye ndiye ameifungia Yanga mabao mengi, 10, kwenye Ligi Kuu msimu huu.

25: Ni namba inayovaliwa na mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, ambaye ndiye kinara wa kuifungia Simba mabao msimu huu akifanya hivyo mara tisa.

2: Ni makipa wawili tu ambao wamefunga bao kwenye mechi inayozikutanisha Simba na Yanga tangu zianzishwe, Iddi Pazi 'Father' 1993 na Juma Kaseja alifunga penalti Simba ilipoibuka na ushindi wa mabao 5-0.

10:00 Muda wa kuanza mechi

11: Namba ya jezi ya mshambuliaji wa Yanga kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma, ambayo haitaonekana uwanjani leo.

25: Idadi ya watu watakaokuwa uwanjani, kwa maana ya wachezaji 22 kwa timu zote mbili, mwamuzi wa kati na waamuzi wasaidizi wawili.

57,000 : Idadi ya mashabiki watakaoingia uwanjani kushuhudia mchezo huo.

51: Pointi ilizonazo Simba kabla ya kuingia uwanjani. Matokeo ya ushindi au kutoka sare yataendelea kuiweka timu hiyo kileleni

49: Pointi za Yanga kabla ya mchezo dhidi ya Simba, Yanga ikishinda mchezo huo itarejea kileleni kwa kuiondoa Simba, ambayo kwa sasa inashikilia usukani wa Ligi Kuu.

10: Namba ya jezi inayovaliwa na mshambuliaji wa Simba, Juma Liuzio, ambaye anacheza mechi ya kwanza ya watani wa jadi tangu asajiliwe na Simba kwa mkopo kutoka Zesco ya Zambia.

11. Namba ya jezi inayovaliwa na mshambuliaji wa Simba Laudit Mavugo, ambaye anatajwa mno kuelekea mchezo huu kutokana na umahiri wa kufumania nyavu aliouonyesha kwenye mechi za karibuni. Amefunga mabao matatu katika mechi tatu za Simba zilizopita.

7000. Kiingilio cha chini cha mchezo wa Simba na Yanga, kwa mujibu wa takwimu mashabiki 36,000 ndiyo watakaokaa kwenye idadi ya viti hivyo.