Simbu, Giniki wang'ara London, Shanghai marathoni

Muktasari:

Nyota hao wa Tanzania wamefanikiwa kuweka rekodi katika mashindano hayo makubwa riadha duniani pamoja na kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanariadha wa Kenya na Ethiopia.
Katika mbio za London marathoni, Simbu alimaliza wa tano akikimbia kwa saa 2:09:10 nafasi sawa na aliyopata kwenye Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016.

Dar es Salaam. Mwanariadha, Alphonce Felix Simbu amemaliza nafasi ya tano katika mbio za London marathoni, mwenzake Emmanuel Giniki akitwaa medali ya dhahabu katika mbio za Shanghai marathoni zilizofanyika Jumapili hii.

Nyota hao wa Tanzania wamefanikiwa kuweka rekodi katika mashindano hayo makubwa riadha duniani pamoja na kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanariadha wa Kenya na Ethiopia.
Katika mbio za London marathoni, Simbu alimaliza wa tano akikimbia kwa saa 2:09:10 nafasi sawa na aliyopata kwenye Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016.

Katika mbio za London, mkenya Daniel Wanjiru alitwaa ubingwa na kujihakikishia kitita cha Dola 100,000 akitumia muda wa saa 2:05:48 akifutiwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia alitumia saa 2:05:57 na Bedan Karoki akiwa wa tatu akitumia saa 2:07:41 na Abel Kirui akiwa wa nne ametumia 2:07:45.
Wakati Simbu akikosa kititam Mtanzania mwingine Giniki aling'ara China kwa kumaliza wa kwanza katika mbio za Shanghai nusu marathoni akitumia saa 01:01:36, huku Mtanzania mwingine, Joseph Panga akimaliza wa sita.
Makocha wa wanariadha hao, Gidamis Shahanga na Francis John wamefurahishwa na matokeo hayo huku wakisisitiza Tanzania imeanza kurejea kwenye enzi zake katika riadha.

"Giniki amejitahidi kwa kuwapita wanariadha wa Kenya na Ethiopia waliomaliza wa pili na watatu, hiyo ni nafasi nzuri kwake, pia ameonyesha 'kukomaa' kwenye ushindani wa kimataifa," alisema Shahanga ambaye ni bingwa wa zamani wa madola wa marathoni.

Kocha wa Simbu, Francis John alisema nafasi aliyopata mwanariadha huyo katika mbio za London si ya kubezwa kwani ni moja ya nafasi nzuri kwenye mbio hizo.

"Kuwa namba tano katika mbio kama za London siyo ya kitoto, ni matokeo mazuri kwa Simbu mwenyewe na taifa na yanatujengea heshima, kuingia hatua ya tano bora si haba," alisema kocha huyo.