Singida United yaibomoa Mbeya City

Muktasari:

  • Kenny amemaliza mkataba na City alikuwa akiwaniwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu wakiwemo wakongwe Simba na Yanga, matajiri wa ligi, Azam FC pamoja na Mbeya City wenyewe, lakini wote hao walishindwa kufikia dau alilokuwa akilihitaji huku Singida United pekee ikifuzu mtihani huo.
  • Meneja wa mchezaji huyo, Maka Mwalwisi alisema kuwa wamekubali ofa hiyo kwani ni ofa nzuri na hivyo timu nyingine ambazo zilikuwa zinamuwania hazitakuwa tena na nafasi ya kumsajili kwa sasa hadi hapo mkataba wake na Singida utakapomalizika.

Dar es Salaam. Singida United leo saa nne asabuhi imemsainisha mkataba wa miaka miwili kiungo wa Mbeya City, Kenny Ally.

Kenny amemaliza mkataba na City alikuwa akiwaniwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu wakiwemo wakongwe Simba na Yanga, matajiri wa ligi, Azam FC pamoja na Mbeya City wenyewe, lakini wote hao walishindwa kufikia dau alilokuwa akilihitaji huku Singida United pekee ikifuzu mtihani huo.

Meneja wa mchezaji huyo, Maka Mwalwisi alisema kuwa wamekubali ofa hiyo kwani ni ofa nzuri na hivyo timu nyingine ambazo zilikuwa zinamuwania hazitakuwa tena na nafasi ya kumsajili kwa sasa hadi hapo mkataba wake na Singida utakapomalizika.

"Simba na Yanga hawakuonyesha ile nia ya kweli, Azam wao walimuhitaji na tulizungumza nao ila ofa yao waliyotoa ni ndogo kuliko hii ya Singida United ndiyo maana tumekubali kusaini mkataba huo, tunaamini hii ni sehemu sahihi kwa Kenny kucheza na ni muda wa yeye kufanya kazi.

"Tuliofanya nao mazungumzo ya mara kwa mara na kutoa ofa zao tumewaambia kuwa sasa dili halitawezekana tena acha mchezaji akatafute maisha sehemu nyingine, Mbeya City wamemlea vizuri na amewatumia vizuri ila sasa haya ni maisha mchezaji pia anatakiwa kuangalia maisha mengine pamoja na kupata changamoto mpya," alisema Mwalwisi.