Siri ya ushindi wa Simbu hii hapa

Mshindi wa medali ya dhahabu wa mbio za Mumbai  Marathon, Alfonce Simbu

Muktasari:

  • Simbu ameshinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Mumbai Standard Chartered Marathon kilomita 42 kwa wanaume akitumia muda wa saa 2:09:32 na kuzawadiwa Dola 42,000.

Arusha. Mshindi wa medali ya dhahabu wa mbio za Mumbai  Marathon, Alfonce Simbu (25) amesema siri ya ushindi wake ni kufanya mazoezi ya kujituma na kuwa na dhamira ya ushindi, hasa baada ya kushika nafasi ya tano  katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Brazil mwaka jana.

Simbu ameshinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Mumbai Standard Chartered Marathon kilomita 42 kwa wanaume akitumia muda wa saa 2:09:32 na kuzawadiwa Dola 42,000.

Akizungumza baada ya kutua Kia, Simbu amesema mbio hizo, hazikuwa rahisi kwa kuwa alikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanariadha wa kimataifa wa Kenya na Ethiopia tangu mwanzo wa mbio.

“Mbio zilikuwa ngumu, njia zao si nzuri, kulikuwa na milima na kona kali, joto pia, lakini nilijiandaa vizuri, nawashukuru makocha wangu, Francis John na Anthony Mwingireza kwa msaada mkubwa walionipa,” amesema Simbu.