Sirro kuimarisha ulinzi Uwanja Taifa

Muktasari:

Kamanda Siiro anasema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unachezwa katika hali ya usalama.

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amewahakikishia mashabiki usalama katika mchezo wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga utakaopigwa Uwanja wa Taifa.
Kamanda Siiro anasema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unachezwa katika hali ya usalama.
“Wananchi wasiwe na wasiwasi wowote wa usalama na pia wote ushirikiano wa kutoa taarifa ya jambo lolote watakaloliona kuwa linaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani kwa kipindi chote watakapokuwa ndani au nje ya uwanja,” anasema Sirro.
Kamanda Sirro anasema kamera maalum za ulinzi za CCTV zitakuwepo ili kuhakikisha sehemu zote za mageti ya kuingilia na kutokea na maeneo yote yanayoonekana ili kuweka kumbukumbu za matukio muhimu.
Anasema hataruhusiwa mtu kuingia na maji, silaha au kitu chochote cha kuhatarisha amani na kutakuwa na kifaa maalum cha kupima kileo kwa yeyote atakayebainika kuwa na kilevi hataruhusiwa kuingia uwanjani.
“Nina usongo na watu wanaotaka kuhatarisha amani kama kuna mtu analengo hilo ni bora akatulia nyumbani, michezo ni amani, michezo ni burudani na michezo ni afya. Kwenye afya hakuna uhalifu,” anasema Sirro.