SportPesa yaipa udhamini mnono Cape Town City

Muktasari:

  • Klabu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita imeingia kwenye makubaliano ya udhamini wa miaka minne na SportPesa watakaokuwa wadhamini wao wakuu kwenye jezi zao pamoja na kuwa washirika rasmi wa klabu hiyo katika michezo ya kubashiri.

Klabu ya Cape Town City inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’ imekuwa klabu ya kwanza kutoka nchini humo kudhaminiwa na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa.

Klabu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita imeingia kwenye makubaliano ya udhamini wa miaka minne na SportPesa watakaokuwa wadhamini wao wakuu kwenye jezi zao pamoja na kuwa washirika rasmi wa klabu hiyo katika michezo ya kubashiri.

Mkurugenzi wa SportPesa Afrika Kusini, Nick Ferguson pamoja na Mmiliki wa klabu ya Cape Town, John Comitis walisaini makubaliano hayo jijini Cape Town leo ijumaa Agosti 11 huku magwiji hao wa michezo ya kubashiri duniani wakitambulisha uwepo wao kwenye Ligi hiyo ambayo inatajwa kuwa ligi tajiri zaidi barani Afrika.

“Tunawakaribisha washirika wetu wa kwanza nchini Afrika Kusini ambao ni Cape Town City FC kwenye familia yetu ya SportPesa. Udhamini huu ni uthibitisho kutoka SportPesa kuwa tumejidhatiti katika kuhakikisha tunachangia maendeleo ya mpira wa miguu kwenye nchi hii.

“Tuna furaha kubwa sana kufanya kazi na Cape Town City FC, klabu ambayo inaendana na thamani yetu na tunatazamia kuwa na kipindi cha

mafanikio ambacho kitahamasishwa na safari hii ambayo tumeianza pamoja”, alisema Ferguson wakati wa sherehe ya kutiliana saini.

Nembo ya SportPesa sasa itakuwa ikionekana upande wa mbele wa jezi rasmi ya Cape Town City FC baada ya timu hiyo kuingia kwenye orodha ya timu kubwa za mpira wa miguu duniani zinazodhaminiwa na kampuni hiyo.

Makubaliano haya yanahusisha timu ya wakubwa, timu B na timu za vijana za Cape Town City, ambayo itashiriki kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika kwa mwaka 2018 baada ya kumaliza nyuma Bidvest Wits na Mamelodi Sundowns katika Ligi ya Afrika Kusini

Klabu hiyo ilianzishwa na mfanyabiashara John Comitis ambaye ni mmiliki wa zamani wa Cape Town Spurs na mwanzilishi wa Ajax Cape Town mwaka 2016 ambapo ndipo Cape Town City FC ilizaliwa upya ikiwa ni miongoni mwa vilabu vilivyotamba nchini Afrika Kusini katika miaka ya 1960 na 1970.