Monday, July 17, 2017

Stars yapewa vigezo vya kufuzu Chan

By Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taifa Stars inahitaji ushindi katika mchezo wake wa marudiano dhidi ya Rwanda ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwenye harakati za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).

Mechi hiyo imetazamwa kwa jicho la tatu na wachezaji wa zamani wa timu hiyo huku wakitaja vigezo ambavyo vinaweza kuiwezesha Stars kufuzu.

Taifa Stars inahitaji ushindi wa aina yoyote katika mchezo huo utakaofanyika Rwanda baada ya kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, juzi jioni na Stars ilisawazisha kwa mkwaju wa penalti.

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema ili Taifa Stars isonge mbele, kocha Salum Mayanga anapaswa kuboresha safu yake ya viungo, ambayo alisema kwa mtizamo wake anaona kama imepwaya.

“Viungo wa Stars wanachokijua ni kukaba na kuokoa, lakini hawana mipango ya kuwatengenezea washambuliaji nafasi za kufunga au kupiga pasi za mwisho, hilo bado ni tatizo,” alisema.

“Japo huwa kuna dhana imejengeka kwamba Stars haina wafungaji, dhana hiyo mimi napingana nayo, tatizo la timu yetu ni viungo kutokuwa na uwezo wa kutoa pasi za mwisho, kocha hakifanikiwa kumaliza tatizo hilo mbona Chan tunakwenda.

“Kocha Mayanga kama kweli anataka kuipeleka Stars Chan basi atilie mkazo katika kuboresha safu ya viungo kabla ya marudiano.”

Mkongwe mwingine, Sekilojo Chambua alisema bado Stars haichezi kitimu, lakini akasisitiza mafanikio ya timu hiyo yatapatikana endapo tu uzalendo halisi kwa wachezaji utaonekana.

“Unajua unapochezea timu ya taifa hiyo ni heshima kubwa, lakini huenda wachezaji wetu wa sasa hawaelewi au wanafanya makusudi, wakiamua kuwa wazalendo na kuonyesha mapenzi na kucheza kwa moyo kwenye timu ya taifa, tutafanya vizuri,” alisema Chambua.

“Lakini kwa sasa naona uzalendo kwa wachezaji bado ni tatizo, lakini pia timu yetu bado haina muunganiko mzuri kitimu, hilo ni jukumu sasa la kocha kulifanyia kazi katika mazoezi yake.”

Endapo Stars itashinda mchezo huo wa maruadiano huko Rwanda, itasonga mbele na kucheza na mshindi kati ya Uganda na Sudan Kusini.

-->