Super Girls mabingwa wa ARS

Muktasari:

Katika mashindano hayo, Mpiruka Queens waliibuka katika nafasi ya tatu baada ya kuwafunga Kipara Queens mabao 2-1

Lindi. Timu ya wasichana ya Super Girls imetwaa ubingwa wa mashindano ya vijana chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars Mkoa wa Lindi baada ya kuichapa FC Vito Malaika mabao 4-1 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Nachingwea.

Katika mashindano hayo, Mpiruka Queens waliibuka katika nafasi ya tatu baada ya kuwafunga Kipara Queens mabao 2-1.

Katika mchezo wa fainali, Super Girls walianza kwa kasi na kuliandama lango la wapinzani wao tangu dakika za mwanzo na kuandika bao la kuongoza dakika ya 15 lilofungwa na Ashura Mfaume baada kugongeana pasi vizuri na Tatu Makota.

Baada ya bao hilo, Super Girls waliendelea kutandaza kandanda safi na kufanikiwa kufunga bao la pili dakika ya 18 lilifungwa tena na Ashura baada ya kuwalamba chenga mabeki watatu wa FC Vito Malaika. Bao la tatu lilifungwa na Alia Fikiri dakika ya 22 baada ya mabeki wa FC Vito kushindwa kuokoa mpira wa kona.

FC Vito Malaika walipata bao lao la kufutia machozi dakika ya 27 baada ya Sarah Isaac kuachia shuti kali na mpira kujaa moja kwa moja wavuni. Hadi mapumziko, Super Girls walikuwa wakiongoza kwa mabao 3-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikasaka bao lakini ilikuwa ni Super Girls waliopata bao dakika ya 63, baada ya Tatu kufunga kwa penalti iliyotokana na beki wa FC Vito Malaika kuunawa mpira ndani ya eneo ya hatari.