TFF: Ratiba FA haina kasoro

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas.

Muktasari:

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alifafanua kwamba umbali ni kutozipangia timu kwenda umbali mrefu tofauti na uchumi wao pia uwezo hawawezi kupanga timu yenye uzoefu na zile ambazo zinaibukia.

Dar es Salaam. Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limeweka wazi kwamba ratiba ya Kombe la FA, (Azam Sports Federation Cup) imezingatia mambo mawili muhimu ambayo ni umbali na uwezo wa timu.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alifafanua kwamba umbali ni kutozipangia timu kwenda umbali mrefu tofauti na uchumi wao pia uwezo hawawezi kupanga timu yenye uzoefu na zile ambazo zinaibukia.

“Lengo ni kuhakikisha soka ya Tanzania, inakuwa kwenye ubora wa hali ya juu, mfano tumeipanga Yanga na Ashanti kwa kuwa imewahi kushiriki Ligi Kuu hivyo ina uzoefu wa kutosha,” alisema Alfred.

Alielezea kwamba michuano hiyo inazipa timu za madaraja ya chini changamoto ya kujituma ili siku moja zije kucheza Ligi Kuu.

“Michuano hii ni mikubwa kwa kuwa mwakilishi wa nchi kwenye ile michuano ya Shirikisho Afrika anapatikana huku na hizi klabu ndogo zimekuwa zikitumia vizuri hii michuano kwa kutaka kuonyesha ubora wao wa kucheza soka ili waonekana kwenye klabu kubwa.

‘’Hii ni nafasi yao na kwa bahati nzuri kwa mwaka huu imekuwa tofauti kwakuwa tumeongeza ushiriki wa timu kwa kuwapa nafasi mabingwa wa mikoa na nia yetu ni moja kama ilivyo kwa Fifa basi na sisi tunataka soka lichezwe kote kwa kulisambaza maeneo tofauti,” alisema Alfred.

Lucas aliongeza kuwa changamoto haziwezi kukosekana ila wanajitahidi kuhakikisha wanazifanyia kazi ili kadri siku zinavyosogea michuano hiyo iwe kwenye kiwango bora ambacho kila mtu atavutiwa nacho ili iweza kurejesha utaratibu wa awali kupata paspoti ndani ya siku saba.

 

Matokeo ya juzi

Kwa mechi zilizochezwa juzi, Yanga ilitumia nafasi hiyo kuiadhibu Ashanti FC mabao 4-1 katika mchezo uliokuwa wa upande mmoja uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mechi nyingine, Mbao FC iliyopanda Ligi Kuu ‘kimazabe’, iliifunga Alliance mabao 2-1 katika mchezo mkali uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.