TFF yaitosa Simba kisomi

Muktasari:

Wachambuzi wa soka nchini pia wametabiri kuwa mchezo huo utaamuliwa na mbinu za mAidha, mchezo huo utakaofanyika Jumamosi jijini Dar es Salaam umetajwa kuamuliwa na mbinu za makocha wa timu hizo, Mcameroon wa Simba, Joseph Omog na Mzambia wa Yanga, George Lwandamina.

Dar es Salaam. Wakati Simba na Yanga zikiingia kambini kujiandaa na mechi ya watani, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa sababu tano za mchezo huo kutochezeshwa na waamuzi wa nje ya nchi kama ambavyo Simba ilitaka.

Aidha, mchezo huo utakaofanyika Jumamosi jijini Dar es Salaam umetajwa kuamuliwa na mbinu za makocha wa timu hizo, Mcameroon wa Simba, Joseph Omog na Mzambia wa Yanga, George Lwandamina.

 

Sababu tano za TFF kuigomea Simba

Simba iliwahi kutamka kutaka mchezo wao na Yanga uchezeshwe na waamuzi kutoka nje ya nchi mara baada ya mchezo wao wa awali wa Ligi Kuu msimu huu kumalizika kwa sare bao 1-1, Simba ikisawazisha na kulalamikia bao la mkono la Yanga lililofungwa na Amiss Tambwe.

“Waamuzi watakaochezesha mchezo huo ni wa hapa hapa nyumbani na watatangazwa Ijumaa, hatuwezi kuleta waamuzi wa nje, kwanza kanuni haziruhusu.

“Pili, hadi kuwaleta lazima wadau saba waridhie ambao ni TFF, Simba, Yanga au timu yoyote itakayocheza na Simba, Chama cha Waamuzi, Kamati ya Ufundi, mashindano na ile ya waamuzi, vinginevyo haiwezekani.

“Tatu ukileta waamuzi wa nje unawaandaaje kisaikolojia hawa wa nyumbani, nne wale wa nje wakikosea unawaadhibu kwa kanuni ipi na mwisho bingwa wa Ligi Kuu haamuliwi kwa mechi ya Simba na Yanga pekee,” alisema Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas.

Ofisa huyo alisema waamuzi wa mechi hiyo ya Jumamosi ni wa hapa hapa nyumbani na si vinginevyo.

 

Makocha watwishwa zigo

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema mshindi wa mechi hiyo ataamuliwa kwa mbinu za makocha wa pande zote mbili. “Hii ni mechi ambayo kwa kiasi fulani itakuwa ni tofauti na mechi kadhaa za Simba na

Yanga za miaka ya hivi karibuni, sababu timu zote mbili ziko juu kwenye msimamo na zinasaka ubingwa wakati zamani kulikuwa na pengo baina yao kwenye msimamo.

“Simba imeanza kuimarika katika safu ya ushambuliali, ambayo imeanza kufunguka tofauti na mechi kadhaa na iliwategemea zaidi viungo, Yanga ipo vilevile ingawa mabao yao yanatokea kulia kwa Juma Abdul na Simon Msuva.

“Huu mchezo utaamuliwa kwa mbinu za makocha, kocha atakayeingia na ‘game plani’ nzuri ndiye ataondoka na pointi tatu siku hiyo kutokana na ubora wa timu zote mbili,” alisema Mayay.

Mchambuzi Joseph Kanakamfumu alisema pamoja na mchezo huo kutotabirika, lakini Simba bado ina tatizo katika safu yake ya ulinzi.

“Kama mabeki wa Simba wakikutana na washambuliaji wasumbufu wataigharimu timu yao, lakini upande wa Yanga pia haipo vizuri katikati lakini pia umri umeenda kulinganisha na viungo wa Simba,” alisema Mayay.

 

Mashabiki nao waanza maandalizi

Mechi ya Simba na Yanga huibua mihemko kwa mashabiki wa pande zote mbili, ambao wameanza maandalizi.

“Yanga ndiyo wameshikilia ubingwa wetu, tunawafunga Jumamosi na kutangaza ubingwa, maandalizi ya kwenda Taifa kuisapoti timu yetu yameanza na tunatarajia kufanya mambo kadhaa kwa jamii kabla ya mchezo huo,” alisema Katibu wa Kundi la Ushangiliaji la Simba la Wekundu wa Terminal, Joel Mwakitalima.

Upande wa Yanga, bosi wa Kundi la Ushangiliaji la Wakali wa Terminal, Steven Mwakilema alisema shamrashamra za mchezo huo zimeanza ikiwa ni pamoja na kuweka tayari ngoma, tarumbeta na dhana nyingine za ushangiliaji.

 

Ndanda, Mtibwa Sugar zashikwa

Katika michezo ya jana za Ligi Kuu Bara, timu ya Ndanda na ilazimishwa suluhu na African Lyon matokeo yanayofana na mechi kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Ruvu.

Mechi kati ya Mbao FC na Majimaji iliyokuwa ichezwe jana imesogezwa mbele.