TFF yatangaza mkakati wa Olimpiki 2020 Tokyo

Muktasari:

TFF ilizindua kampeni hiyo lengo ni kuhakikisha Tanzania inaingiza timu kwenye michezo hiyo ambayo itahusisha maandalizi ya timu ya vijana chini ya miaka 15 ambayo kambi yake iko jijini Mwanza, timu ya Taifa chini ya miaka 17 Serengeti Boys na vijana waliopatikana baada ya michuano ya Ligi ya vijana chini ya miaka 20 iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Dar es Salaam. Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likizindua kampeni ya kuelekea Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan 2020, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Soka, Kim Poulsen amesema maandalizi ya mapema na matumizi sahihi ya muda ndivyo vitakavyoivusha Tanzania kwenye michezo hiyo.
TFF ilizindua kampeni hiyo lengo ni kuhakikisha Tanzania inaingiza timu kwenye michezo hiyo ambayo itahusisha maandalizi ya timu ya vijana chini ya miaka 15 ambayo kambi yake iko jijini Mwanza, timu ya Taifa chini ya miaka 17 Serengeti Boys na vijana waliopatikana baada ya michuano ya Ligi ya vijana chini ya miaka 20 iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Akizungumza katika mahojiano maalumu baada ya uzinduzi huo, Poulsen alisema: “Ninawashuku TFF kwa mikakati hii, tumebakiwa na miaka miwili, 2017 na 2018 kwa kuwa 2019 mechi za kufuzu zitaanza, haitakiwi kujivuta.
“Tunatakiwa kucheza mechi nyingi za kirafiki na timu zenye uzoefu, ninaamini tukiyapa kipaumbele mambo hayo hatutakwama katika safari hii, lakini kama haitakuwa mikakati ya dhati, hakuna kitakachofanyika,” alisema Poulsen.
Poulsen alisema pia kuwa safari ya 2020 si ya mtu mmoja, inatakiwa kuwa na ushirikiano na kila mdau ili kuleta mafanikio.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Ofisi za TFF, Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi alisema shirikisho linahitaji kuungwa mkono na wadau wote katika mkakati huo ili kufanikisha azma ya Tanzania kufuzu kushiriki michezo hiyo.
“Tuna timu ya U-15 kule Mwanza, tuna vijana wa Serengeti Boys na tuna vijana tuliowapata kwenye mashindano ya U-20. Mpango huu una gharama kubwa, tunaomba kampuni mbalimbali, mashirika na wadau kuunga mkono juhudi hizi.
“Tumeanzisha Mfuko wa Maendeleo Soka kusaidia upatikanaji wa rasilimali. Juhudi zote hizi pia zinalenga kuhakikisha Tanzania inafuzu fainali za Kombe la Dunia za 2026,” alisema Malinzi na kupiga kijembe akisema: “Watu wanaojipanga kuwania uongozi wa TFF baadaye mwaka huu lazima wajiweke sawa.”
Akichangia katika mkakati huo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuf Omari Singo alisema wachezaji wanapaswa kudumisha nidhamu ili kufikia lengo linalotarajiwa na kuwaletea mafanikio binafsi.
“Vijana hiyo ni fursa yenu, mjitahidi kuwa na nidhamu ili mfike mbali. Tushirikiane katika vikao mbalimbali ili tuende pamoja,” alisema Singu na kusisitiza umuhimu wa TFF, TOC na wadau kushirikiana ili kutimiza azma hiyo.
Mtazamo wadau
Mchezaji wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka Ally Mayay alisema, Mfuko wa Maendeleo ya Soka umekuwapo tangu nchi ilipopata uhuru, lakini haujasaidia katika harakati za kuinua soka. “Anachozungumza Poulsen ndicho kinafanywa na nchi zilizo makini na maendeleo ya soka. TFF ni watu, mfumo huo umekuwapo kwa muda mrefu, lakini sioni tija yake. Kama ni suala la kutafuta rasilimali, Serikali ichukue jukumu la kuusimamia ili ufanikishe malengo yaliyokusudiwa,” alisema Mayay.
Mshambuliaji wa zamani Prisons, Osward Morris alisema umakini katika kusimamia mipango na mikakati utaivusha Tanzania katika safari ya kuelekea Tokyo 2020.
Rufani ya Serengeti
Malinzi alitumia hafla hiyo kuchombeza kuwa rufani ya Serengeti Boys dhidi ya Congo Brazzaville huenda ikapatiwa ufumbuzi na Shirikisho la Soka Africa (CAF) mwishoni mwa wiki hii.
“Tuvute subira, moshi mweupe unaweza kuonekana Libreville wiki hii, tuna matumaini makubwa,” alisema Malinzi.

Kagera yamuenzi Burhan
Kagera Sugar imemuenzi kipa wake David Burhan aliyefariki jana kwa kuifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Katika mchezo huo uliogubikwa na huzuni ya msiba wa kipa Burhan wenyeji Kagera ilipata mabao yake yalifungwa na Mbaraka Yusuph na Twaha Ibrahimu wakati Stamili  Mbonde alifunga bao la kufutia machozi kwa Mtibwa Sugar.
Katika mchezo mwingine JKT Ruvu ililazimishwa suluhu na Stand United kwenye Uwanja Mkwakwani, Tanga.