Taifa Stars yaichapa Burundi

Taifa Stars yaichapa Burundi

Muktasari:

Katika mchezo huo mabao ya Stars yalifungwa na Saimon Msuva na Mbaraka Yussuf wakati lile la kufutia machozi la Burundi lilifungwa na Laudit Mavugo.

Dar es Salaam. Taifa Stars imeendeleza makali yake chini ya kocha Salum Mayanga baada ya kuifunga Burundi kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo mabao ya Stars yalifungwa na Saimon Msuva na Mbaraka Yussuf wakati lile la kufutia machozi la Burundi lilifungwa na Laudit Mavugo.

Stars iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Jumamosi dhidi ya Botswana.

Kinara wa ufungaji wa Ligi Kuu Bara, mshambuliaji wa Yanga, Msuva alifungia Stars

 bao la kuongoza dakika 20, akiunganisha krosi ya Mohammed Hussein iligongwa kwa kichwa na Ibrahim Ajib kabla ya kumkuta mfungaji aliyepiga shuti lililojaa wavuni.




Bao hilo la Stars lilidumu hadi mapumziko kipindi cha pili na Burundi ilirudi kwa kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji wa Simba, Mavugo katika dakika ya 54, baada ya beki wa Stars, Abdi Banda kukosea kuokoa mpira uliokuwa ukielea langoni kwake.




Baada ya bao hilo Burundi ilitawala mchezo huo, lakini mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mayanga ya kumtoa Farid Mussa na kumwingiza Yussuf yalizaa matunda katika dakika 78, alifunga bao la pili baada ya kupiga shuti lililogonga mwamba na kumalizia tena wavuni na hadi filimbi ya mwisho, Tanzania ilishinda mabao 2-1.
Kocha Stars, Mayanga alisema amefurahishwa na matokeo hayo.


"Si kwamba tumecheza vibaya, lakini nikiri timu yangu ilikuwa na uchovu, wachezaji wamefanya kazi kubwa na lengo letu ni kuangalia timu itakayokwenda katika mashindano ya CHAN,"alisema Mayanga.

Katika mechi za kusaka kufuzu kwa  fainali za CHAN 2018 zitakazofanyika Kenya, huku Tanzania imepangwa na Rwanda na mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam Julai 14 na marudiano Julai 21 jijini Kigali.

Tangu ilipofuzu kwa CHAN 2009 nchini Ivory Coast, Tanzania imeshindwa kufuzu kutokana na ubutu wa safu ya ushambuliaji wa ndani.