Tunisia yaichapa Algeria

Muktasari:

Katika mchezo huo wa jana jioni, uliokuwa na ushindani mkubwa Tunisia ilipata mabao yake kupitia beki wa Algeria, Msakni aliyejifunga akijaribu kuokoa krosi ya Mnadi kabla ya Sliti kufunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti wakati Algeria ilipata bao la kufutia machozi katika dakika 90, lililofungwa na Sofianne.

Libreville, Gabon. Tunisia imejiweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa Algeria mabao 2-1.

Katika mchezo huo wa jana jioni, uliokuwa na ushindani mkubwa Tunisia ilipata mabao yake kupitia beki wa Algeria, Msakni aliyejifunga akijaribu kuokoa krosi ya Mnadi kabla ya Sliti kufunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti wakati Algeria ilipata bao la kufutia machozi katika dakika 90, lililofungwa na Sofianne.

Kwa matokeo hayo ya mchezo wa mapema wa Kundi B umeifanya Tunisia kufikisha pointi nne na kuongoza kundi kabla ya mechi ya Zimbabwe dhidi ya Senegal.

Majeruhi watikisa Ghana, Misri

Beki wa Ghana, Baba Rahman na kipa wa Misri, Ahmed El Shenawy wamelazika kuyaacha mapema mashindano ya Mataifa ya Afrika 2017 kutokana na kuwa majeruhi.

Beki wa Ghana, Baba (22) aliumia goti wakati wa mchezo wa Black Stars kwanza walioshinda 1-0 dhidi ya Uganda, Jumanne iliyopita.

Mchezaji huyo alilazimika kutolewa mapema uwanjani kutokana na maumivu hayo na hakuna aliyetegemea kwamba hali ingekuwa hivyo hadi alipopelekwa hospitali mjini Libreville na kubaini amepata majeruhi makubwa.

Rahman amerudisha Ujerumani katika klabu yake ya Schalke 04 kwa uchunguzi zaidi katika mji wa Gelsenkirchen.

Wakati Ghana wakipata pigo hilo Misri nayo itamkosa kipa wake namba moja, Ahmed El Shenawy katika mashindano hayo kutokana na kuumia.

Kipa huyo aliumia wakati wa mchezo wa Kundi D dhidi ya Mali baada ya kujigonga kwenye goli na kulazimika kutolewa nje.

Vipimo vya X-ray vimeonyesha kwamba amepata tatizo la misuri hivyo atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa wiki mbili.

Misri sasa imebakiwa na kipa moja mkongwe, Essam El Hadary baada ya kipa Sherif Ekramy kuumia hivyo hataweza kucheza dhidi ya Uganda kesho.