UKOCHA: Pluijm amwaga mboga Yanga

Muktasari:

  • Uongozi wa Yusuf Manji akiwa Yanga haujawahi kukaa na kocha huyo kwa misimu miwili au zaidi

Dar es Salaam.  Usemi wa Waswahili kuwa, ukimwaga ugali, nami namwaga mboga umetimia kwa klabu ya soka ya Yanga  ambayo licha  ya uongozi wake jana kukanusha kuajiriwa kwa kocha Mzambia George Lwandamina na kuachana na Mdachi Hans van der Pluijm, mzungu  huyo ametangaza kujiuzulu kazi hiyo.

Mapema jana,  katibu mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alisema uongozi wao hauna taarifa  za ujio wa Lwandamina wala haujafanya mawasiliano yoyote na mkufunzi huyo. “Kwanza, hizo taarifa nasikia kwako, hatujazungumza naye na wala hatujui kama amekuja, anaweza kuwa amekuja kwa shughuli zake. Kocha Yanga ni Hans Pluijm,” alisema Baraka.

Lwandamina alikanusha akisema kwamba ujio wake nchini hauna maana kwamba amekuja kusaini mkataba Yanga, ingawa alikiri kwamba timu hiyo inamhitaji na kama ikichangamka yuko tayari kufanya kazi nchini.

Sababu za uamuzi wa Pluijm

Akizungumza uamuzi wake wa kujiuzulu, Pluijm alisema uwapo wa kocha huyo nchini umemchukiza na kuamua kumuandikia mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji barua ya kujiuzulu nafasi yake.

Pluijm alisema hajafurahishwa na mambo yalivyokuwa yakifanyika na kwamba licha ya uongozi wa klabu yake wakati wote kukanusha hawana mpango na Lwandamina, lakini anao uhakika wako katika mazungumzo na kocha huyo wa Zesco United.

Alisema kuna nafasi Yanga walitaka kumpa, lakini ameshindwa kukubaliana nayo kutokana na mambo yalivyofanyika.

Pluijm alitajwa kubadilishiwa wadhifa na kuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Lwandamina. “Unajua hakuna siri katika dunia ya sasa, sijafurahi mambo yalivyokuwa yanafanyika hawakutanguliza heshima kwangu, nimewaandikia barua ya kujiuzulu ili waniache niondoke vyema,” alisema Pluijm na kuongeza: “Sikupanga kuondoka Yanga kwa ubaya, lakini hili sikulifurahia, nawashukuru wanachama na mashabiki pamoja na uongozi na wachezaji wangu kwa kunipa nafasi ya kufanya kazi hapa na kesho (leo) nitakwenda kuwaaga wachezaji wangu,” alisema Pluijm.

Jana asubuhi, Pluijm alisema hana nafasi ya kuzungumzia ujio wa Lwandamina na kusisitiza kuwa kwa sasa anahitaji kutuliza akili kwani anasubiri taarifa rasmi.

Huku akicheka Pluijm alisema: “Nimesikia mengi, yameandikwa na kusemwa juu yangu kuondoka Yanga, lakini najiamini, mimi ni kocha mwenye kiwango, nimefanya kazi kubwa Yanga na ninazidi kuendelea kufanya, ingawa sishangazwi na yanayosemwa kwani vitu kama hivyo ni kawaida kutokea duniani.

“Nimeifanyia Yanga vitu vingi tangu iliponiajiri hadi sasa, kama kuna mabadiliko nitaambiwa na waajiri wangu, nami nitaeleza misimamo wangu.”

Wengine wanasemaje

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema kuondolewa kwa Pluijm hashangazwi nako kwani ndivyo mpira ulivyo kokote duniani. “Hata Mourihno (Jose) alitimuliwa Chelsea, hivyo ni kawaida ya makocha, lakini mimi sioni udhaifu wa Pluijm naangalia mafanikio aliyowapa Yanga hadi imecheza mashindano ya kimataifa na kufika mbali tu,” alisema Mayanja.

Mwanasoka wa zamani wa Yanga na Pan African ambaye pia ni kocha, Mohammed Adolph ‘Rishard’ alisema timu kucheza mfululizo kwa kiwango kile kile ni ngumu hivyo haoni sababu ya Yanga kumuondoa Pluijm.

“Sioni kama Yanga iko katika kiwango kibovu nafikiri ni uchovu kwani hata ukiangalia Azam  ndiyo tatizo linalowasumbua, timu haiwezi kucheza misimu miwili mfululizo kwa kiwango kile kile, sasa wanapobadilisha kocha wategemee mambo mawili, timu kuendelea kuwa kama ilivyo au kuzidi kuporomoka zaidi,” alisema Rishard.