USAJILI: Hanpoppe awatega Mkude, Ajibu

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe

Muktasari:

  • Yumo Said Ndemla ambao mikataba yao Simba inakaribia mwisho

Dar es Salaam. Wakati wakiwa kwenye  kiwango kizuri msimu huu na kutakiwa sana hasa kwenye mchezo ujao dhidi ya watani zao, Yanga, Oktoba Mosi, wachezaji nyota watatu wa Simba, kiungo na nahodha  Jonas Mkude na mshambuliaji Ibrahim Ajibu wanasikilizia ofa kutoka ndani na nje ya klabu hiyo baada ya mikataba yao kukaribia mwisho.

Pamoja na wawili hao, pia kiungo Said Ndemla amebakiza miezi minne kuanza mazungumzo na timu nyingine kuhusu kusaini mkataba mpya  wa kubakia Simba au la.

Akizungumzia hatima ya wachezaji hao Simba, mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspoppe alisema  kuwa kuendelea kuitumikia timu hiyo kupo mikononi mwa wachezaji wenyewe.

Nyota hao ambao wamekuwa tegemeo kwenye kikosi cha Simba msimu huu wamebakiza miezi minne kuanza mazungumzo na timu nyingine kwa ajili ya usajili mpya kulingana na kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Wachezaji hao kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili jana kuwa hawapo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia mikataba mipya sasa Simba.

“Kwa sasa siwezi kuzungumzia suala la mkataba mpya, tusubiri huu wa sasa utakapomalizika kwanza,” alisema Mkude.

Ajibu ambaye amekuwa akihusishwa na klabu mbalimbali ikiwamo Yanga alisema: “Ninachokiangalia sasa ni kuitumikia timu yangu, wakati utakapofika kila kitu kitajulikana, lakini siyo sasa, bado nina mkataba na Simba.”

Ndemla ambaye amekuwa akichezeshwa mara chache akitokea benchi alisema suala la mkataba mpya kwake ni la baadaye kwani sasa anaendelea kutumikia mkataba alionao, wakati ukifika kila kitu kitajulikana.

Wakati wachezaji hao wakitoa kauli hizo, bosi wa usajili  wa klabu ya Simba (Hanspoppe) alisema baada ya mikataba ya nyota hao kumalizika wenyewe wataamua  kuendelea kuitumikia timu hiyo au kuondoka.

“Mikataba yao inakwisha Juni mwakani, hivi sasa bado ni wachezaji wa Simba kwa mujibu wa mkataba, lakini wakati ukifika, tutakaa nao na kujua muelekeo wao,” alisema Hanspoppe na kuongeza:

“Tunajua kanuni zinamruhusu mchezaji kufanya mazungumzo na timu nyingine katika kipindi cha miezi sita kabla ya mkataba wake wa awali kumalizika, lakini ninachoweza kusema hivi sasa ni mapema kuzungumzia mipango ya klabu na wachezaji husika.

“Sisi (Simba) tuna malengo yetu na wachezaji tulio nao, lakini huwezi kujua mchezaji, huenda akawa na malengo yake tofauti, kwa kuwa bado ni wachezaji wetu kwa sasa, tuwaache kwanza hadi mikataba yao itakapomalizika.

“Wakati ukifika tutakaa nao, tutazungumza, tuwasikie wao wanasemaje, lakini si kwa sasa tuache waichezee Simba,” alisisitiza  kigogo huyo wa usajili wa klabu ya Simba.

Kuhusu  mipango wa kuboresha kikosi chao wakati wa dirisha dogo baadaye mwaka huu,  Hanspoppe alisema hilo litafanyika kulingana na matakwa ya kocha mkuu, Joseph Omog na benchi lake la ufundi.

Lyanga aula  Uarabuni

Siku moja baada ya mshambuliaji Dan Lyanga kudaiwa kujiunga na Fanja FC ya Oman, Simba imeibuka na kueleza kuwa mshambuliaji huyo bado ni mali yao.

Lyanga amejiunga na Fanja juzi baada ya kufuzu majaribio kwenye klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Oman. Mshambuliaji huyo msimu huu ameshindwa kuhimili ushindani wa namba kwenye kikosi cha kwanza.

Kinyume na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mshambuliaji huyo amesajiliwa moja kwa moja na Fanja, Simba  imeeleza kuwa bado Lyanga ni mali yao, amepelekwa huko kwa mkopo.

Ofisa habari wa Simba, Haji Manara aliliambia gazeti hili jana kuwa uongozi wa klabu hiyo  umempa baraka zote mshambuliaji huyo ili kuitumikia Fanja.

“Wapenzi na mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi na taarifa hizo za Lyanga kuiacha Simba, yeye bado ni mchezaji wetu na amejiunga na timu ile kwa mkopo na si kama tumemuuza.

Simba, Majimaji Uwanja Taifa

Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamekubali ombi la Simba la kucheza mechi zake uwanja wa Taifa.

TFF imetangaza jana kuwa mechi mbili za raundi ya sita za Ligi Kuu ile ya Simba na Majimaji, na African Lyon na Kagera Sugar zitachezwa kwenye uwanja huo badala ya Uwanja wa Uhuru.

 Mabadiliko hayo yametokana na TFF kusitisha kwa muda kutumia Uwanja wa Uhuru katika kipindi hiki ambacho imeanza kufanyia marekebisho sehemu ya uwanja huo ambayo ni ya nyasi bandia (artificial turf).

Awali Simba waliomba kutoutumia tena Uwanja wa Uhuru (Shamba la Bibi), wakiorodhesha sababu tatu.

Sababu hizo ni hofu ya usalama wa afya ya wachezaji kutokana na plastiki zinazoshika nyasi bandia kukauka, uwanja kuwa mdogo na uchakavu wa plastiki zilizowekwa kwenye nyasi hizo za bandia uwanjani hapo walizodai zimechangia baadhi ya wachezaji wao kuumia.