Ubingwa Simba upo hapa

Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya (kulia) akipongezwa  wachezaji wenzake wa Frederick Blagnon na Mohamed Hussen (kushoto) baada ya kufunga bao la pili dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Simba ilishinda mabao 2-0. Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

  • Ni zile zitakazofanyika jijini Dar es Salaam ambazo lazima ipate matokeo mazuri ikiwamo dhidi ya Yanga, Azam kwenye mzunguko wa pili

Dar es Salaam. Kimahesabu ni kama mlima mrefu, lakini kama rekodi ya msimu uliopita itafanya kazi, Simba ina mechi 12 muhimu, sawa na pointi 36 za kupigania ili  kuibuka na ushindi  na pengine kutwaa ubingwa msimu huu, ikimaliza ukame wa wake wa zaidi ya misimu mitatu.

Timu hiyo iliyocheza mechi tisa hadi sasa,  huku ikiongoza ligi kwa pointi 23, inapaswa kuhakikisha inaibuka na ushindi kwenye 12 itakazocheza jijini Dar es Salaam, zikiwamo dhidi ya Yanga na Azam, ambako ndiko kuliifanya ikose ubingwa msimu uliopita.

Msimu uliopita, Simba ilipoteza pointi 19 kwenye mechi ilizocheza Dar es Salaam wakati mikoani ilipoteza pointi tisa pekee.

Iwapo Simba ingepata pointi kwenye mechi dhidi ya Toto Africans, Mwadui, Majimaji na Prisons na kisha kupata pointi nne tu kati ya 19 ilizopoteza nyumbani, ingefanikiwa kutwaa ubingwa.

Pengine, pointi hizo ilizopoteza nyumbani (Dar es Salaam), zingeiwezesha (Simba) kutwaa ubingwa kwani ilimaliza ligi ikiwa na pointi 62 wakati mtani wake, Yanga iliyotwaa ubingwa ikimaliza na pointi 73, yaani tofauti ya pointi 11.

Mechi hizo 12 zilizobaki ambazo Simba itachezea Dar es Salaam ni mbili dhidi ya African Lyon, Mbao FC, Toto Africans, Prisons, Mbeya City, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mwadui FC, Stand United, Yanga na Azam.

Kwa kulitambua hilo, timu hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha inaibuka na ushindi kwenye mechi zilizobaki itakazocheza Dar es Salaam pia kulinda rekodi yao ya msimu uliopita ugenini.

Waziri wa zamani wa Michezo na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya ambaye pia ni mdau mkubwa wa timu hiyo, aliliambia gazeti hili kuwa anaamini kuwa iwapo watafanya vizuri kwenye mechi zote zitakazochezwa jijini, Simba itatwaa ubingwa.

“Kwanza, hali ya hewa ya hapa wameizoea, lakini pili ndipo kuna viwanja vizuri kwa mechi pamoja na mazoezi kulinganisha na mikoani.

“Pia, Simba ikicheza hapa inakuwa na mashabiki wengi ambao wanahamasisha wachezaji kufanya vizuri. Tunataka kuhakikisha hatupotezi pointi hata moja kwenye mechi zote za nyumbani ambazo naamini ndizo zinaweza kutupa au kutunyima ubingwa,” alisema msomi huyo.

Profesa Kapuya alisema kuwa Simba ina kila sababu ya kutwaa ubingwa msimu huu kutokana na kikosi chake kuwa kizuri kulinganisha na misimu iliyopita.

“Kwanza,  kikosi chetu kina muunganiko mzuri wa kiuchezaji ndani ya uwanja, lakini pia ni kipana kwa maana kuwa waliopo ndani na wale wanaokaa benchi wote ni wazuri.  Mchezaji anaweza kutokea benchi na akafanya vizuri kuliko yule aliyeanza,” alisema Profesa Kapuya.

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Ally Mayay alisema, Azam na Yanga zitakuwa na wakati mgumu kwa Simba kwenye mzunguko wa pili.

“Bado ligi ni ‘mbichi’, lakini kwa viashiria vya sasa na namna Simba inavyojengeka na kuwa moja ya timu mbili ambazo hazijafungwa tangu kuanza kwa msimu huu, kuna dalili ya ugumu kwa Yanga na Azam katika ndoto zao za kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.

“Hii ni ishara kwamba, msimu huu Simba haitaki kufanya makosa, hivyo kama Yanga na Azam zisipojipanga, mzunguko wa pili zitakuwa na kazi ya ‘kuifukuza’ Simba,” alisema Mayay.

Akizungumzia mwelekeo wa Stand ya Shinyanga ambayo inaungana na Simba kuweka rekodi ya kutokufungwa hadi sasa, Mayay alisema kama  itaweza kuendeleza rekodi hiyo hadi mwishoni mwa Desemba, timu hiyo itaingia katika orodha ya timu shindani, lakini siyo sasa.

“Stand inafanya vizuri, inajitahidi, lakini kama kweli itamudu kuendeleza rekodi hiyo hadi Desemba mwishoni, hapo ndipo itaweza kuingia katika orodha ya timu zilizodhamiria kumaliza katika nafasi za juu msimu huu,” alisema Mayay.