Udhamini Mbao FC waizindua Toto

Muktasari:

Mbao FC ilipata udhamini huo mwishoni mwa wiki iliyopita ambao utamalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi.

Dar es Salaam. Udhamini wa Sh25 milioni ambao timu ya Mbao FC ya hapa imeupata kutoka Kampuni ya Hawaii Product umewashtua jirani zao, Toto Africans ambao wameingia msituni kusaka kampuni za kuwadhamini.

Kampuni hiyo (Hawaii) imeidhamini Mbao FC inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 16 kupitia bidhaa yake ya maziwa ya unga ya Cowbell.

Mbao FC ilipata udhamini huo mwishoni mwa wiki iliyopita ambao utamalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi.

Ofisa habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet aliliambia gazeti hili kuwa timu yake imepeleka maombi kwa kampuni 40 tofauti nchini kwa ajili ya kuomba udhamini kwa timu hiyo.

“Hadi sasa kati ya hizo kampuni 40, kuna moja ambayo tayari tulishaanza mazungumzo nayo na yanaelekea kumaliza. Nadhani wao ndio wana nafasi kubwa ya kuwa wadhamini wetu ingawa sitoweka wazi hiyo kampuni.

Kuhusu Mbao FC, sisi (Toto Africans) tunawapongeza kwa udhamini huo walioupata kwa sababu utawasaidia kufanya vizuri kwenye ligi.

“Kama unavyojua kuwa timu zetu kwa muda mrefu zimekosa wadhamini hivyo kitendo cha Mbao kupata udhamini, kitasaidia kufungua milango kwa watu wengine,” alisema Japhet.

Mara ya mwisho kwa Toto kupata udhamini kwenye Ligi Kuu ilikuwa mwaka 2011 ambako ilidhaminiwa na Jarida la 4-4-2.