Uganda Cranes yaaga Afcon mapema

Beki wa Simba Mganda, Murushid Juuko (kushoto) akiokoa mpira huku kipa wake Denis Onyango (chini) akijaribu kumzuia mshambuliaji wa Misri, Marwan Mohsen wakati wa mchezo wa fainali za Mataifa ya Afrika uliofanyika mjini Port-Gentil. Uganda ilifungwa bao 1-0. Picha na AFP.

Muktasari:

Abdallah Said aliingia akitokea benchi na kuifungia Misri bao pekee katika dakika 90 na kuwafanya Mafarao hao kuwa katika nafasi nzuri ya kuungana na Ghana kufuzu kwa robo fainali, wakati Cranes wakiwa tayari wameanga mashindano.

Port-Gentil, Gabon. Uganda imeanga mashindano ya Mataifa ya Afrika 2017 baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Misri katika mchezo wa pili wa Kundi D.

Abdallah Said aliingia akitokea benchi na kuifungia Misri bao pekee katika dakika 90 na kuwafanya Mafarao hao kuwa katika nafasi nzuri ya kuungana na Ghana kufuzu kwa robo fainali, wakati Cranes wakiwa tayari wameanga mashindano.

Misri ilionekana kuwa ipo makini katika mashambulizi yake ya kushtuki ikiwatumia washambuliaji wake Mohamed Salah na Ramadan Sobhi, lakini safu ya ulinzi ya Uganda ikiongozwa kipa Dennis Onyango ilikuwa makini.

Uganda ikicheza kwa kujiamini tofauti na mchezo wa kwanza ilitegeneza nafasi nyingi za kufunga lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kutumia nafasi hizo kufunga.

 Katika dakika ya 28, nusura beki wa Misri, Ahmed Hegazy ajifunge mwenyewe wakati akijaribu kuzuia krosi ya beki wa kushoto wa Uganda, Joseph Ochaya.

Cranes nusura ipate bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza wakati shuti la Farouk Miya aliyegongena pasi na Tony Mawejje lilipotoka nje kidogo ya goli.

Awali Ghana ilijihakikisha kufuzu kwa robo fainali baada ya kuichapa Mali kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Port-Gentil.

Nahodha wa Black Stars, Asamoah Gyan alifungia Ghana bao pekee katika kipindi cha kwanza lilitosha kuwapa pointi tatu.

Mali inayonolewa na kocha Alain Giresse pamoja na kipigo hicho imeendelea kubaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi moja itasubiri mechi yake ya mwisho kuamua kama itafuzu kwa robo fainali au la.Uganda inamaliza mashindano hayo Jumatano kwa kucheza na Mali wakati vinara wa Kundi D, Ghana wataonyeshana kazi na Misri.

Vikosi

Misri: Essam El Hadary, Ahmed Hegazy, Ali Gabr, Mohammed Abdel Shafi, Ahmed Fathi, Mohamed Elneny, Ramadan Sobhi (Amr Warda 66’), Mahmoud Hassan (Mahmoud Abdel-Moneim 80’), Tarek Hamed (Abdallah Said 59’), Mohamed Salah, Marwan Mohsen

Uganda: Dennis Onyango, Joseph Ochaya, Murushid Juuko, Godfrey Walusimbi, Denis Iguma (Moses Oloya 90+1’), Hassan Waswa, Farouk Miya (Nicholas Wadada 81’), Khalid Aucho, Geoffrey Kizito, Tony Mawejje, Geoffrey Massa (Muhammad Shaban 65’).