Usajili wa Yanga wa kimataifa zaidi

Muktasari:

Nyika amesema mashabiki wa soka nchini watambue kuwa Yanga imelikamata soka la Tanzania kwa sasa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Yanga, Hussein Nyika amesema klabu hiyo imefanya usajili madhubuti wenye lengo la kuhakikisha wanafanya vizuri kimataifa.

Nyika amesema mashabiki wa soka nchini watambue kuwa Yanga imelikamata soka la Tanzania kwa sasa.

"Kamati imefanya kazi kubwa, Yanga inalenga kuliteka soka la Afrika na si hapa nyumbani tu. Wanachama wa Yanga waondoe hofu kuhusu timu yao," amesema Nyika katika mahojiano yaliyofanyika makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Jangwani.

Katika kipindi hiki cha usajili Yanga imewasajili Ibrahim Ajibu, Abdallah Shaibu, Ibrahim Yahya  na kufanikiwa kuwabakisha mastaa Donald Ngoma na Thaban Kamusoko.

Katika hatua nyingine, Nyika alibinisha kuwa klabu hiyo imekamilisha usajili kwa asilimia 95.

"Leo (Alhamisi) tunamalizana na Tshishimbi muda wowote kwakuwa amefuzu vipimo vya afya. Asilimia tano iliyobaki tutasajili wachezaji wa ndani," alisema

Mmoja wa wachezaji wanaohusishwa kumwaga wino ni Raphael Daud wa Mbeya City.

Nyika alisema mazungumzo kati ya pande mbili yanakwenda vizuri.