Uwekezaji mpya Yanga wenye utata

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji

Muktasari:

Mkataba wa ukodishwaji wa klabu hiyo licha ya kuorodhesha vipengele vitatu vitakavyoineemesha klabu hiyo iwapo vitafanyiwa kazi, baadhi yake ama vilivyopo havijawekwa wazi na kuibana Yanga.

Dar es Salaam. Ni dhahiri Yanga imekaribisha uwekezaji mkubwa, ambao bila umakini inaweza kutumbukia kwenye shida ambazo itakuwa vigumu kujiondoa.

Mkataba wa ukodishwaji wa klabu hiyo licha ya kuorodhesha vipengele vitatu vitakavyoineemesha klabu hiyo iwapo vitafanyiwa kazi, baadhi yake ama vilivyopo havijawekwa wazi na kuibana Yanga.

Mjumbe wa zamani wa kamati ya utendaji ya Yanga na nahodha wa timu hiyo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kibiashara, Ally Mayay aliliambia gazeti hili jana kuwa mkataba huo wa ukodishwaji una faida kubwa na utaipa maendeleo iwapo itatekelezwa ipasavyo.

“Klabu inapoanzishwa ni lazima iwe na malengo ya msingi ambayo watu wanakuwa wamejiwekea. Wakati klabu hizi zilipoanzishwa miaka zaidi ya 80 iliyopita, malengo yao makuu kwa wakati ule yalikuwa ni kusaidiana na kujumuika pamoja.

“Nyakati hizi malengo yamebadilika na kuna vitu lazima viangaliwe zaidi ya hayo malengo ya kuanzishwa miaka hiyo. Katika miaka ya sasa mwanachama anatakiwa apewe kipaumbele na kunufaika na uwepo wa timu yake,” alisema.

“Mwanachama anatakiwa kupata kipaumbele cha kuingia uwanjani kuitazama timu yake pia anataka kuona timu yake inapata matokeo mazuri,” aliongeza.

Mayay alisema kuwa ukodishwaji huo wa Yanga una faida kwa wanachama kwa sababu utawapatia kile wanachokihitaji.

Wanachama watakuwa na uhakika wa kupata matokeo mazuri kama mkataba unavyosema na pia watakuwa na uhakika wa kuwa na timu imara yenye wachezaji wazuri, haitatoa kiasi chochote mfukoni kwani hilo ni jukumu la mkodishwaji.

Pia, Yanga itaweza kuendesha shughuli nyingine kama kustawisha matawi ya wanachama kutokana na faida itakayopatikana kwenye mkataba,” alisema Mayay.

Hata hivyo, Mayay alionyesha wasiwasi wake kwenye kipengele cha 3.3, akieleza kuwa ingawa kina manufaa bado maelezo yake hayajitoshelezi.

Kipengele hicho kinasema,” Mkodishwaji atailipa Yanga katika mwaka wa fedha wowote ule kukiwa kuna faida ya fedha taslimu, asilimia 25 ya fedha ambayo Yanga itaitumia kujenga uwanja wake. “

“Sawa, Yanga itapata fedha kiasi hicho, lakini bado mkataba haujafafanua kuwa baada ya miaka 10 ya kumalizika kwake, nani atasimamia matumizi ya faida hiyo.

“Kumbuka hapo mkodishaji atairudishia Yanga, jina na nembo yake sasa, je nani atakayesimamia? Hapo mkataba haukuweka wazi,” alisema Mayay.

Kipengele kingine ni kile cha mkodishaji kuipa Yanga kiasi cha Sh100 milioni kwa mwaka ili klabu hiyo iwekeze kwenye kuimarisha mtandao wa matawi.

Yanga imekuwa na fedha za udhamini wa Azam Tv kila msimu, zaidi ya Sh100 milioni ambacho hivi karibuni kiliongezeka hadi kufikia Sh126 milioni.

Hata hivyo, Mayay alisema kuwa hakuna tatizo kwa Yanga kupewa fedha hizo kwa sababu haitokuwa na mzigo mkubwa.

“Kumbuka wakati huo gharama zote zinazohusu timu hazitokuwa za Yanga, bali mkodishwaji tofauti na sasa kiasi kama hicho ambacho mdhamini anakitoa, kinatakiwa kutumika kwenye usajili, kulipa mishahara na posho za wachezaji pamoja na huduma nyingine kwa timu,” alisema.

Pia, Mayay alisisitiza kuwa, Bodi ya Wadhamini Yanga, inapaswa kusimama imara kuhakikisha mkataba huo unaleta tija kwa klabu kama mchanganuo wake ulivyo.

Hata hivyo, katika mkataba huo, kipengele kingine kinachokosekana ni kile kinachotaja eneo la Gezaulole Kigamboni, ambako Yanga ilikabidhiwa juzi kwa ajili ya uwekezaji.