Vigogo VPL ulimi nje FA

Wachezaji wa Mwadui FC.

Muktasari:

  • Kiwango bora cha uwanjani kilichoonyeshwa na baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, kilizilazimu timu za Ligi Kuu kutumia nguvu ya ziada kupata matokeo ya kufuzu hatua ya 16.

Dar es Salaam. Wakati Mwadui FC na Ruvu Shooting zikiaga Kombe la Shirikisho la Azam, mechi za raundi ya tano za mashindano hayo zilizochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, nusura zikate vichwa zaidi vya baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Kiwango bora cha uwanjani kilichoonyeshwa na baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, kilizilazimu timu za Ligi Kuu kutumia nguvu ya ziada kupata matokeo ya kufuzu hatua ya 16.

Pamoja na matarajio ya kupata mchekea mbele ya timu za Daraja la Kwanza, hali ilikuwa tofauti na zikajikuta zikipata matokeo kwa tabu.

Mshangao ulikuwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi ambako Ruvu Shooting waliduwazwa a Kiluvya United ya Daraja la Kwanza kwa mabao 2-1, wakati mkoani Mwanza, Mwadui FC ilikuwa timu ya pili ya Ligi Kuu kufungishwa virago kwa penati 5-4 na Toto Africans.

Kwenye Uwanja wa Uhuru, Simba ilitumia uzoefu kuifunga Polisi Dar mabao 2-0.

Kocha msaidizi wa Simba, Iddi Salim alikiri kuwa kiwango walichoonyesha dhidi ya Polisi Dar hakikuwa kizuri.