Wachezaji vibonge kwa Guardiola imekula kwao

Muktasari:

 Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amepiga marufuku wachezaji wenye uzito mkubwa kufanya mazoezi na wenzao kwenye klabu hiyo.

Shenzhen, China. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amepiga marufuku wachezaji wenye uzito mkubwa kufanya mazoezi na wenzao kwenye klabu hiyo.

Badala yake amesema wachezaji hao watalazimika kwenda kliniki kupima uzito.

Kocha huyo pia amepiga marufuku wachezaji wake kula pizza na amewaonya wenye uzito mkubwa kuwa atawaondoa kikosini.

Guardiola aliyeanza kibarua Manchester City wiki tatu zilizopita, aliwaeleza uamuzi  huo wachezaji wake  alipokuwa akiwazuia wasitumie vinywaji vyenye kiasi kikubwa cha sukari.

Bosi huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich anatambulika kwa umakini wake mkubwa katika mazoezi na mechi.

Beki Gael Clichy amefichua msimamo huo wa bosi wake mpya, akisema ndiyo umekuwa sehemu ya maisha yao tangu kocha huyo atue klabuni hapo.