Wadau waiuma sikio Takukuru suala la rushwa uchaguzi wa TFF

Muktasari:

  • Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana juu ya uchaguzi huo ambao utahusisha wagombea wa nafasi ya Urais, Umakamu wa Rais na wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF, wadau hao walisema kuwa mbinu pekee ya kupata viongozi bora ni kudhibiti rushwa kwenye uchaguzi huo.

Historia ya chaguzi mbalimbali kutawaliwa na rushwa imewapa hofu wadau wa soka nchini na kuiomba taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) kuziba mianya ya wagombea rushwa katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa shirikisho la soka Tanzania (TFF) utakaofanyika Agosti 12, mkoani Dodoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana juu ya uchaguzi huo ambao utahusisha wagombea wa nafasi ya Urais, Umakamu wa Rais na wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF, wadau hao walisema kuwa mbinu pekee ya kupata viongozi bora ni kudhibiti rushwa kwenye uchaguzi huo.

"Ni jambo lililo wazi kuwa wagombea kwenye chaguzi mbalimbali iwe za kisiasa au za michezo kama soka wamekuwa wakitoa rushwa kwa wapiga kura kama mbinu ya kuwashawishi jambo ambalo limekuwa likisababisha kupata viongozi wasiostahili," alisema mjumbe wa kamati ya mashindano ya Yanga, Athuman Kihamia.