Wagonjwa wa Yanga wazua hofu

Obrey Chirwa

Muktasari:

  • Yanga na Simba zitapambana Agosti 23 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni kuashirikia kuanza kwa Ligi Kuu

Dar es Salaam. Majeruhi na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji kunaweza kuwa pengo kubwa kwa Yanga inayojiandaa kuikabili Simba.

Yanga na Simba zitapambana Agosti 23 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni kuashirikia kuanza kwa Ligi Kuu

Timu hizo kwa sasa ziko visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo huo, Simba ikiweka kambi Unguja na Yanga ikiwa Pemba.

Mzizi wa hofu

Achana na usajili wa nyota wengi iliyoufanya Simba, lakini hali ya majeruhi imeanza kuwapa hofu mashabiki wa Yanga.

Simba wanacheka wakiamini kuwa wapinzania wao wana majanga, lakini moja ya timu hizo ikiwa na kasoro hupata matokeo.

Obrey Chirwa, Geofrey Mwashiuya na kipa Beno Kakolanya wote ni wagonjwa na wamebaki Dar es Salaam kwa matibabu na mazoezi maalumi, hivyo hawatacheza mchezo huo.

Pia, kipa Youth Rostand naye bado hajawa fiti akitoka kwenye majeruhi licha kuwapo kambini na kuanza mazoezi mepesi.

Hiyo inamaanisha kuwa maombi yote ya mashabiki wa Yanga yatakuwa kwa Rostand, wakiomba awe fiti na afya njema kabla ya mchezo huo kwani kama haitakuwa hivyo, basi golini ataanza chipukizi, Ramadhan Kabwili wa Serengeti Boys ambaye bado hajaaminika.

Pengo la Msuva

Ukubali ukatae, pengo la Saimon Msuva litakuwepo kwenye mchezo huo kwani winga huyo alikuwa chachu ya ushindi wa Yanga katika mechi nyingi msimu uliopita zikiwemo za watani wa jadi.

Licha ya kwamba mashabiki walikuwa wakimzomea katika mchezo baina ya Simba na Yanga, lakini bado Msuva aliendelea kuwa mchezaji muhimu kikosini na Agosti 23, kocha George Lwandamina anatakiwa akune kichwa kupata mtu sahihi wa kuziba pengo lake ili Yanga ipate ushindi.

Mchezaji wa zamani ya Yanga, Ally Mayai alisema huu ni wakati wa kocha Lwandamina kuonyesha umuhimu wake.

“Mechi za Simba na Yanga huwa ni 50 kwa 50 na mara nyingi kinachoamua mechi ni utimamu wa akili kwa wachezaji. Unaweza ukawaandaa wachezaji kimwili lakini pia wanatakiwa waandaliwe kiakili.

“Ukweli Yanga kunaweza kukawa na upungufu na changamoto, hivyo kocha ndiyo wakati wa kuonyesha umahiri wake.

“Kutokuwapo kwa Msuva ni pengo kwani bado Yanga inategemea mipira ya krosi. Tambwe ili afunge anategemea krosi, hivyo nani atakuwa mbadala wa Msuva? Hapo ndipo kocha anatakiwa kuonyesha umahiri kwani Chirwa ni mgonjwa,” alisema Mayai.

Aliongeza: “Pia, kutokuwepo kwa Bossou (Vincent) kutapunguza utulivu kwenye safu ya ulinzi ya Yanga.”

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema Yanga inaweza kunufaika na Ibrahim Ajib kama kocha atamtumia katika sehemu sahihi.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Yanga, Dismas Ten alisema mashabiki wa Yanga hawapaswi kuwa na hofu kwani timu ipo vizuri.

“Majeruhi ndio hao watatu, lakini wachezaji wengine wote wapo vizuri wanaendelea na mazoezi,” alisema Ten.